Hatimae shirikisho la soka nchini TFF, limetangaza tarehe za michezo ya hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

TFF wametangaza Aprili 20 na Aprili 21, 2018 ni tarehe maalum ya michezo hiyo, ambayo itakuwa na jibu la nani na nani watatinga kwenye hatua ya fainali ya michuano hiyo, ambayo bingwa wake ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika CAF mwaka 2019.

Nusu fainali ya Kwanza itachezwa Ijumaa Aprili 20,2018 ikiwakutanisha Stand United ya Shinyanga watakaokua wenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Kambarage,Shinyanga saa 10 jioni.

Singida United ya Singida watawakaribisha JKT Tanzania ya Dar es Salaam kwenye nusu fainali ya pili itakayochezwa Uwanja wa namfua Jumamosi Aprili 21,2018 saa 10 jioni.

Washindi kwenye nusu fainali hizo watacheza mchezo wa fainali May 31,2018.

Ikumbukwe kuwa Stand Utd walitinga hatua ya nusu fainali baada ya kuifunga Njombe Mji bao moja kwa sifuri, huku Mtibwa Sugar wakiwagalagaza Azam FC kwa mikwaju ya penati tisa kwa minane, baada ya timu hizo kwenda sare katika muda wa kawaida.

Kwa upande wa Singida Utd waliwafunga mabingwa wa soka Tanzania bara Young Africans kwa mikwaju ya penati nne kwa mbili, huku JKT Tanzania wakiichabanga Tanzania Prisons mabao mawili kwa sifuri.

Samia Suluhu azindua kampeni ya kujikinga na Saratani ya shingo ya kizazi
Kambi ya Twiga Stars yavunjwa