Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amekabidhi barua yake ya kujiuzulu akiachia madaraka wakati kukiwa na maandamano makubwa dhidi yake baada ya miongo miwili ya uongozi wake.

Kelele za shangwe na honi za magari zilisikika jijini Algiers kabla ya watu waliobeba na kupeperusha bendera za Algeria kutoka majumbani mwao na kumiminika mitaani wakishangilia habari ya kujiuzulu kwa rais Abdelaziz Bouteflika.

Barua ya kujiuzulu kwake iliyoonekana na shirika la habari la serikali APS, imemnukuu Bouteflika akisema hatua aliyoichukua anatumai itatoa nafasi kwa Algeria kusonga mbele na kuwa na mustakabali mwema.

Aidha, Algeria kwasasa inapitia kipindi cha mpito baada ya rais huyo kujiuzulu, na maswali juu ya nini kitafuata kwa taifa hilo tajiri kwa gesi na mshirika wa Magharibi katika kupambana na Ugaidi yameanza kuibuka.

Hata hivyo, Katiba ya Algeria inasema rais akifariki dunia au kujiuzulu baraza la katiba ni lazima lithibitishe, kabla ya mabunge yote mawili kukutana na spika wa bunge kuteuliwa kama rais wa mpito kwa siku 90, wakati uchaguzi wa rais ukiandaliwa. Kwa hiyo moja kwa moja Abdelkader Bensalah aliye na miaka 77 mshirika wa Bouteflika ambaye ndiye spika wa bunge la sasa nchini Algeria ndiye rais wa mpito.

Makala: Siri nzito ya Afande Sele na Ufalme wa Rhymes, vilio na shangwe #TBT
Upinzani wasusia bunge hukumu ya Lema, watoka nje