Serikali ya Jamuhuri Ya Muungano wa Tanzania imeagizwa kufanya uchunguzi wa ‘Fedha za Mchina’ zinazokatwa katika mapato ya kila mchezo unaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Agizo hilo kwa Serikali, limetolewa na Bunge linaloendelea mjini Dodoma kupitia ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka ujao wa fedha iliyosomwa na mjumbe wa kamati hiyo, Deogratius Ngalawa.

Bunge pia limeitaka serikali kuhakikisha kuwa na udhibiti wa mapato ya michezo ya soka kwa kuuza tiketi kwa mfumo wa kieletroniki, baada ya kubainika fedha nyingi zimekuwa zikipotea, unapotumika mfumo wa kawaida.

Ngalawa amesema kamati yao inatambua mapato ya Uwanja wa Taifa na Uhuru ni makubwa lakini nchi inakabiliwa na tatizo la udanganyifu katika taarifa za mapato hayo.

“Kumekuwa na fedha zinazojulikana kwa jina la fedha za Mchina kwa kila mchezo kwa kuwa wamekuwa wakilipwa Wachina wanaohudumia uwanja,” amesema Ngalawa.

Mbunge huyo wa Ludewa (CCM) ameongeza: “Kamati imehoji kuhusu suala hili lakini haijapata maelezo ya kuridhisha, hivyo inashauri uchunguzi ufanywe kuhusu fedha za Mchina zinazokatwa katika kila mchezo na Bunge lako tukufu lipewe taarifa.”

Amesema kamati yao pia imeshauri mapato ya Uwanja wa Taifa na Uhuru yasichanganywe, baada ya kubainika yamekuwa yakichanganywa kwa makusudi ili kuleta mkanganyiko kwa wadau.

Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu udanganyifu wa mapato ya mechi za soka nchini huku serikali ikichukua hatua mbalimbali bila mafanikio ya kutosha.

Unai Emery kufungasha virago Parc des Princes
Vijana wa miaka 12 kwenda Urusi