Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeitaka kampuni ya Acacia kulipa kiasi cha shilingi trilioni 424 kutokana na malimbikizo ya kodi tangu mwaka 2000, kwa makampuni yake tanzu ya Bulyanhulu Gold na Pangea Minerals.

Kwa wastani wa bajeti ya Tanzania ya mwaka jana ambayo ni trilioni 31, kiasi hicho cha deni la kodi ni sawa na bajeti ya miaka 13.

Deni hilo limetokana na matokeo ya ripoti mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza sakata la usafarishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi uliokuwa ukifanywa na kampuni hiyo.

Hata hivyo, Acacia imekana madai hayo ya TRA kwa maelezo kuwa bado hawajapewa ripoti ya kamati hizo mbili licha ya kuziomba tangu zilipotolewa.

“Sisi hatuyakubali makadirio haya. Kampuni itaangalia haki na namna zote zilizopo kuhusu suala hili,” imeeleza taarifa ya Acacia.

Tangu ripoti za tume mbili zilizochunguza sakata hilo kuwekwa wazi, Acacia wamekuwa wakipinga kukwepa kodi na kwamba siku zote imekuwa ikitoa taarifa sahihi kuhusu kiwango cha madini na aina ya madini yaliyoko kwenye mchanga unaosafirishwa kwenda nje ya nchi.

Kwa upande wa TRA, Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipakodi, Richard Kayombo alisema kuwa bado hajapata waraka wowote anaoweza kuutumia kujibu madai ya Acacia hivyo hayuko tayari kutoa moni yoyote.

CCM Kibaha kuwachuja wasaliti, yawaonya kuchukua fomu za uchaguzi wa ndani
RC Mtaka atoa mbinu mbadala kufikia uchumi wa kati Simiyu