Misri wamefuzu fainali za kombe la dunia 2018, wakitokea ukanda wa bara la Afrika. Walipangwa katika kundi la tano (E) sambamba na mataifa ya Uganda, Ghana na Congo Brazzaville katika mashindano ya kuwania nafasi hii.

Misri walimaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi hilo kwa kufikisha alama 13, wakiwaacha Uganda waliokuwa na alama 9, nafasi ya tatu ikashikwa na Ghana kwa alama 7 na Congo Brazzaville waliburuza mkia kwa kuwa na alama 2.

Jina la utani la timu ya taifa ya Misri: The Pharaohs

Mfumo: Kikosi cha Misri hutumia mfumo wa 4-2-3-1.

Image result for 2018 fifa world cup: Mohamed Salah GhalyMchezaji Nyota: Mohamed Salah Ghaly (Liverpool).

Image result for 2018 fifa world cup: Mahmoud Hassan “Trézéguet”Mchezaji hatari: Mahmoud Hassan “Trézéguet” (Anacheza kwa mkopo Kasımpaşa, akitokea Anderlecht).

Image result for 2018 fifa world cup: Héctor Raúl CúperKocha: Héctor Raúl Cúper (62), raia wa Argentina.

Ushiriki: Misri wameshiriki fainali za kombe la dunia mara mbili, mwaka 1934 na mwaka 1990, hii ni mara ya tatu. Iliweka historia ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kushiriki fainali hizi.

Mafanikio: Hatua ya makundi (Mwaka 1990).

Kuelekea 2018:

Misri hupendelea kucheza mfumo wa kuzuia na kufanya mashambulizi ya kushtukiza, na hali hiyo imekifanya kikosi chao kuwa na safu imara ya ulinzi.

Kikosi cha Misri kimesheheni wachezaji chupukizi na wenye uzoefu kama mlinda mlango Essam El-Hadary ambaye mwaka huu atafikisha miaka 45.

Safu yao ya ulinzi inajengwa kwa ushirikiano wa Rami Rabia na beki wa klabu ya West Brom ya Uingereza, Ahmed Hegazi.

Sehemu ya kiungo kuna Mohamed Elneny wa Arsenal ya Uingereza na Abdallah Said wa klabu ya Al Ahly ya Misri.

Misri inaelekea katika fainali za kombe la dunia huku ikichagizwa na mafanikio alioyapata Mohamed Salah katika msimu wake wa kwanza akiwa na Liverpool iliomsajili mwanzoni mwa msimu wa 2017/18, akitokea AS Roma ya Italia.

Salah amemaliza msimu wa ligi ya England akiwa mfungaji bora wa msimu kwa kufunga mabao 32 katika michezo 36 aliocheza, na kutwaa tuzo ya kiatu cha dhahabu, ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu wa chama cha wachezaji wa kulipwa nchini England (2017–18 PFA Players’ Player of the Year), sambamba na kutajwa katika kikosi bora cha msimu ckupitia chama hicho.

Ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa chama cha waandishi wa habari za michezo England na tuzo ya mchezaji bora wa Liverpool msimu wa 2017/18.

Wegine wanaotegemewa katika safu ya ushambuliaji ni Ramadan Sobhi, Kahraba na Mahmoud Hassan “Trézéguet”.

Misri imepangwa katika kundi la kwanza sambamba na wenyeji wa fainali hizo Urusi, Saudi Arabia na Uruguay.

Itaanza kampeni za kuusaka ubingwa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Uruguay katika uwanja wa Central, mjini Yekaterinburg Juni 15, kisha watapambana na wenyeji Urusi mjini Saint Petersburg, uwanja wa Krestovsky Juni 19, na watamaliza michezo ya hatua ya makundi Juni 25 dhidi ya Saudi Arabia, uwanja wa Volgograd, mjini Volgograd.

Misri wana historia ya kuwa nchi iliyokaa miaka mingi zaidi tangu washiriki fainali za kwanza hadi fainali za pili, yaani tangu mwaka 1934 hadi mwaka 1990 ni miaka takribani 56.

Tegemeo la Salah kuipandisha Misri kama afanyavyo kwa Liverpool lipo kwenye kila moyo wa shabiki wa nchi hiyo kwenye kombe hilo.

Mpira ni dakika 90 na zile zitakazoongezwa yakitokea ya kutokea, huenda Misri wakatunisha misuli na kuwakata ngebe za awali wenyeji Urusi, hakuna binadamu aijuaye kesho!

Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi fupi kila siku hapa Dar24, usisahau kutembelea YouTube Channel yetu ‘Dar24media’ upate historia ya matukio yaliyojiri kwenye kombe hili kupitia kipindi cha ‘Zaidi’.

Tunakusogeza karibu na Urusi hadi tushuhudie atakayebeba Kombe la FIFA.

Ramadan Kareem.

Guardiola amwaga wino tena Man City
Tafiti: Vifo 85,000 vya watoto wachanga husababishwa na kukosa maziwa ya mama. 

Comments

comments