Aliyekua bingwa wa mbio fupi duniani Usain Bolt anatarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza wa majaribio katika medani ya soka mwishoni mwa juma hili, akiwa na klabu Central Coast Mariners ambayo imeweka dhamira ya kumsajili.

Bolt ambaye kwa kipindi kirefu amekua na ndoto za kucheza soka la ushindani anatazamiwa kuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo inayoshiriki ligi ya nchini Australia, katika mchezo wa kirafiki dhidi ya wachezaji wa ndani wa nchi hiyo (Local Amateurs).

Kocha wa Mariners Mike Mulvey, amesema bingwa huyo wa medali nane za dhahabu za michuano ya Olimpiki anatarajia kucheza kwa dakika kadhaa kwenye mchezo huo, ambao utaonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya Fox Sports.

Bolt, ambaye alianza kufanya mazoezi yake ya kwanza na kikosi cha Central Coast Mariners juma lililopita, amesema anatarajia kucheza kwa dakika 15 ama 20, na atatumika kama mshambuliaji wa pembeni.

“Kwangu, ni kama kujiweka sawa kimwili kabla ya kuanza kucheza soka kisawa sawa,” alisema mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 32 alipoongea na vyombo vya habari baada ya mazoezi yaliyofanyika kwenye uwanja wa Central Coast mapema leo Jumanne.

“Bado nina nafasi ya kufanya makubwa katika soka, lakini kwa kipindi hiki ni mwanzo wa kutaka kutimiza ndoto zangu, nitaanza taratibu hadi nitakapokuwa tayari kupambana kwa dakika 90.”

Image result for Usain Bolt in Central Coast Mariners

Mwaka jana Bolt aliwahi kufanya mazoezi na kikosi cha klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa msaada wa kampuni ya vifaa vya michezo ya Puma inayoidhamini klabu hiyo, ikiwa ni sehemu ya kutimiza ndoto zake za kujichanganya na wachezaji mashuhuri ili kuzoea mchezo wa soka.

Bolt, pia ni shabiki mkubwa wa klabu ya Man Utd, na mara kadhaa amewahi kuonekana akiwa amevaa jezi ya klabu hiyo, ambayo aliwahi kusema angependa kuitumikia kama mchezaji katika siku za maisha yake.

Vita dhidi ya ufisadi yapamba moto nchini Kenya
Guedes atimka jumla Paris Saint-Germain (PSG)