Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Eliud  Mwaiteleke kuitisha kikao na wananchi wa Kigongo na kutafuta ufumbuzi wa tatizo la eneo la kujenga soko.

Majaliwa amesema hayo leo Juni 21, 2017 wakati akizungumza na mamia ya wakazi na wajasiriamali wanaotumia kivuko cha feri cha Kigongo waliokuwa wakimsubiri avuke kwenda Busisi, wilayani Sengerema.

“Mkurugenzi haya mambo ya mipango, mipango na kupanga hayaleti tija kwa wananchi. Hivi hamjui kuwa wananchi wanahitaji kuwa na soko katika eneo hili ili waweze kuuza mazao yao au samaki?”

“Ninakuagiza Mkurugenzi, kesho Alhamisi, saa 4 njoo na Afisa Biashara wako, Mwenyekiti wa kijiji na watu wako pamoja na Diwani wa hapa, itisheni kikao na muonyeshwe eneo la soko ili mliingize kwenye mipango yenu,” amesema.

Amesema Serikali ya awamu ya tano haitaki kusikia lugha za michakato wakati wananchi wanaendelea kuteseka.

Kabla ya Waziri Mkuu kutoa agizo hilo, alimwita Mkurugenzi huyo ili aeleze amejipanga vipi kwenye Halmashauri yake kutatua tatizo la soko kwa wananchi wa Kigongo.

Mwaiteleke amemwambia Waziri Mkuu kuwa hawajawahi kupata mpango kutoka kwenye kata hiyo na kwa hiyo akawasihi wananchi waibue mpango huo na kuuwasilisha kwenye Halmashauri ili wao waweze kutenga fedha za kujenga soko.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigongo, Sebastian Kisumo amemweleza Waziri Mkuu kwamba eneo hilo linakabiliwa na tatizo la soko pamoja na uhaba wa maji, ambapo Waziri Mkuu amesema Serikali imetenga sh. bilioni 2.5 kwa ajili ya mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria eneo la Itelele ambao utasambaza maji kwenda Misungi,  Usagara hadi Kigongo Feri.

Askari wawili wa usalama barabarani wauawa kwa risasi Kibiti
RC Mghwira ashindilia msumari shamba la Mbowe kuondolewa miundombinu