Watuhumiwa wa ugaidi wanaoshikiliwa katika magereza jijini Arusha leo wametishia kugoma kufika tena mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi zao, wakidai kuwa upelelezi wa kesi yao umechukua muda mrefu.

Kwa mujibu wa kituo cha runinga cha Azam TV, watuhumiwa hao waliofikishwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Arusha, wameiambia Mahakama hiyo kuwa huenda wakagoma kufika mahakamani hapo endapo kesi zao hazitaanza kusikilizwa.

Hata hivyo, Hakimu wa Mahakama hiyo aliwataka watuhumiwa hao kuendelea kufika mahakamani kama kawaida kwani mashauri yao yanaendelea kushughulikiwa. Aliwataka kufika Mahakamani ili waweze kufahamu mwenendo wa kesi zao.

Katika hatua nyingine, watuhumiwa hao wameomba kutohusishwa na matukio ya mauaji yanayoendelea katika wilaya ya Kibiti, wakidai kuwa kauli za baadhi ya viongozi wanaowahusisha na tukio hilo zinawapa wasiwasi kuwa huenda ni chanzo cha kucheleweshwa kusikiliza kesi zao.

Watuhumiwa hao walikamatwa kwa makosa ya ugaidi takribani miaka minne iliyopita na kupandishwa kizimbani. Upande wa Jamhuri unaendelea kukamilisha upelelezi wa mashtaka yao.

Mrisho Mpoto atangaza fursa kwa wasanii
Uamuzi Wa Kikao Cha Kamati Ya Utendaji