Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema zinahitajika juhudi za pamoja za ndani ya nchi, za kikanda na kimataifa katika kuweka mikakati na kutafuta njia madhubuti za kulinda na kuhifadhi bahari na rasilimali zake kwa kusimamia matumizi endelevu ya bahari.
Dkt. Mpango ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam hii leo Juni 8, 2023 na kutaka uwepo wa uwiano sawia kati ya hali ya bahari, kuimarika kwa uchumi kwani Afya ya Bahari na mifumo imara ya kiikolojia ya baharini kwani ni muhimu kwa uchumi wa buluu ambao ni sehemu ya ajenda ya nchi kufikia maendeleo endelevu.
Amesema, umuhimu wa kulinda bahari na rasilimali zake unatokana na faida lukuki zinazopatikana zikiwemo Bahari kuchukua zaidi ya asilimia 70 ya eneo la dunia, zaidi ya asilimia 50 ya hewa safi ya oksijeni, zaidi ya 90% ya joto la ziada linalosababishwa na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuchukua zaidi ya asilimia 30 ya hewa ya Kaboni inayozalishwa na shughuli za kibinadamu.
Dkt. Mpango ameongeza kuwa tafiti zinaonesha kufikia 2030 Bahari itakuwa ndio nguzo kuu ya uchumi duniani ambapo takriban watu milioni 40 watakuwa wameajiriwa moja kwa moja na viwanda vinavyotumia rasilimali za bahari.