Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Karim Benzema huenda akavuta mkwanja mrefu zaidi ndani ya Al Ittihad mpaka kufikia euro 600m.

Imefahamika kuwa Benzema imesaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Al Ittihad ya nchini Saudi Arabia, baada ya kumalizana na Real Madrid ya Hispania kwa miaka kadhaa.

Awali iliripotiwa kuwa, staa huyo mkataba wake kwa mwaka thamani yake itakuwa ni euro 100m na atasaini mkataba wa miaka miwili, lakini pia atakuwa na madili mengine.

Mpango wa timu ambayo inamsajili Mshambulaiji huyo ilikuwa ni kumpa miaka miwili lakini itamuongeza mmoja wa zaidi ambao kama atakaa kwa muda huo basi atalipwa kiasi cha euro 600m.

Al Ittihad wanataka kuona staa huyo anakaa mpaka mwaka 2026 na ataweza kupata kiasi hicho cha fedha akiwa katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia.

Benzema anakuwa staa wa pili kutua ndani ya ligi hiyo, baada ya Cristiano Ronaldo ambaye Januari mwaka huu alijiunga na Klabu ya Al Nassr.

Hata hivyo, kumekuwa na taarifa kwamba Serikali ya Saudi Arabia imetenga kiasi cha dola bilioni 20 kwa ajili ya kuendeleza soka katika ligi yao na mpango ni kusaini nyota wenye majina makubwa.

Benzema akiwa njiani kucheza ligi hiyo msimu ujao, Lionel Messi naye anatajwa kuhitajika na Klabu ya Al Hilal iliyomuwekea dau la euro 400m kwa mwaka, lakini mpaka sasa staa huyo bado hajafanya uamuzi timu gani atachezea msimu ujao.

Wakati yakiendelea hayo ikiwa tunaelekea kipindi cha usajili wa majira ya joto, huenda mastaa wengine wakatua Saudi Arabia kama Sergio Ramos, Sergio Busquets, N’Golo Kante, Pierre-Emerick Aubameyang na Angel Di Maria.

Watatu kuondoka Azam FC 2023/24
Dkt. Mpango ataka juhudi ulinzi wa bahari, rasilimali