Serikali imeagiza Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji kote nchini kutojihusisha na mauzo ya viwanja na vipande vya ardhi na kusema zoezi hilo litakuwa likisimamiwa na Maofisa ardhi kwa kushirikiana na Kampuni za upangaji na upimaji wa ardhi kwenye maeneo na miji husika.
Agizo hilo, limetolewa hii leo Desemba 22, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa akitoa tathmini ya siku 100 za utekelezaji wa Wizara yake tangu alipoteuliwa kushika wadhifa wa Waziri mwenye dhamana na masuala ya ardhi.
Silaa pia amewataka Wananchi kutonunua ardhi ambayo haijapimwa na kuongeza kuwa, “kwa wale wanaokwenda kununua viwanja vijijini hakikisha umeitishwa mkutano wa Kijiji kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa uamuzi wa kupewa ardhi na ikiwezekana tumia simu kurekodi kwa kukubaliwa kupewa hilo eneo.”
Aidha, Waziri Silaa amesema Wizara yake itashirikiana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na wataendelea kupokea na kuheshimu ushauri wanaoutoa kuhusu shughuli za sekta ya ardhi nchini.