Taasisi za kijamii Nchini, zimehimizwa kuweka mkazo katika elimu ya ufundi na ujasiriamali, ili kupata mwarobaini wa tatizo la ajira na kuzalisha wataalamu wengi wa fani mbalimbali.
Rai hiyo, imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi – CCM, Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana katika Mkutano Mkuu wa 10 wa Jukwaa la Vijana wa Kiislamu Mkoa wa Arusha – JUVIKIBA.
Amesema, endapo taasisi za kijamii zitajikita kuhamasisha elimu ya amali (ufundi), vijana wengi watapata utaalamu katika fani mbalimbali ambao utawawezesha kujiajiri, kuajiri wenzao na hata kuwa na sifa ya kuajiriwa katika maeneo mbalimbali ya fani walizozisomea na kujifunza.
Kinana pia aliwapongeza JUVIKIBA kwa kujitoa kupambania elimu ya ujasiriamali na ufundi, ambapo amesisitiza kuwa anaamini jitihada hizo zitawalipa matunda mema kwa kujiingizia kipato badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini.