Kiuhalisia kwasasa ni kweli maisha yamebadilika na kila tunapoamka, tunasikia habari mbaya za mauaji, kibaya zaidi ni yale yanayohusisha watu wa karibu kama Wanandoa, Ndugu wa damu na hata marafiki na visa vyao vunakuwa vya kusikitisha ama kutafakarisha.

Hata hivyo, kuna watu wana majibu juu ya hili na huenda kwa namna moja ama nyingine wanahusika katika kuleta mabadiliko endapo watalivalia njuga kwa kushirikiana na mamlaka husika za utawala wa kiserikali na jamii nzima, hawa ni Wazee.

Wanasemaje.

Kwa vipindi tofauti Wazee wanasema Familia nyingi, mipaka kati ya mke na mme imeondoka, matokeo yake hakuna kusikilizana, vifua vya wanandoa vimejaa hasira, visasi na kutegeana.

Baadhi ya Familia zinahusisha mtu na mzazi mwenzie na siyo mtu na mke ama mume wake, ndani ya Nyumba kila mtu mbabe, hakuna anayesali kwa ajili ya mwenzake, kila mtu anamuombea mwenzake mabaya na kila mtu anamwambia mwenzake kuwa, ipo siku atamtambua.

Pia Familia nyingi, ile mipaka kati ya mzazi na mtoto haipo, leo usishangae kuona mtoto anamfokea mzazi wake tena mbele ya watu, watoto wanataka kuishi bila kuwasikiliza wazazi tofauti na zamani ambapo watoto kabla hawajaamua jambo, walipenda kwanza kupata maoni ya wazazi.

Jamii yetu sasa haihubiri upendo, haihubiri unyenyekevu, haihubiri upatanisho, inahubiri zaidi mali utajiri tena utajiri wa kuupata hata kwa ncha ya upanga.

Kosa lilianzia wapi?

Je, ni pale ambapo jamii iliamua kuanza kukumbatia ubinafsi kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja au kuna sababu nyingine?

Hivi leo inaonekana ni jambo la kawaida mtu hajaonana na ndugu zake wala kuwasiliana nao kwa muda mrefu, achilia mbali kutembeleana.

Iko wapi ile jamii ambayo watoto walikuwa siyo wa mtu binafsi bali wa jamii nzima? Leo hii ukimkaripia mtoto asiye wako kazi unayo.

Matokeo.

Matokeo yake, watoto kukua na tabia zisizoeleweka na hata huko kwenye ndoa tulipoondoa kipengele cha familia ni mali ya jamii nzima, sasa watu hawaogopi kuwa wataonekanaje.

Tatizo lingine ni hili la kuamini kuwa mafanikio kwenye maisha ni kuwa na pesa tu na si vinginevyo, jambo hili limeleta kiburi na ujuaji mwingi usio na tija kwa mtu mmoja mmoja, familia na kuondoa ubinadamu.

Upuuzwaji wa Mila.

Huwezi bisha, ni wazi kuwa sasa tumezikataa mila na desturi zetu za asili, kwani koo nyingi kwasasa hazifahamiani na yale makutano ya mara kwa mara yaliyolenga kujadiliana na kuelimishana namna ya kuishi kwa amani na upendo hayapo tena.

Kila mmoja na lake na hofu zimetoweka, utii kwa wazee haupo! Kuna kipindi pia niliwahi msikia rafiki yangu akisema kuna Wajinga wa zamani ambao walikuwa hawana adabu hivi sasa nao wameingia kwenye kundi la Kuzeeka (Wazee).

Hivyo kwa sehemu yao hawaisaidii jamii zaidi ya kuipotosha kwa maelekezo  yasiyo na mashiko, sina hakika kama hii nayo ni moja ya pointi au kilikuwa ni kibonzo tu!?

Nini kifanyike.

Ni vyema tukajitafakari na kumuomba MUNGU ili TUBADILIKE na kurudia utu wetu, zile hadithi zetu za “BATA KAVAA RAIZONI” hazikuwa sawia bali zilitujenga kiakili na kimtazamo katika kutafuta suluhu ya mambo na kukuza akili, tuache kuhoji eti “Hivi ni kweli Kuku alipanda Baiskeli?” zitakuwa ni kejeli kwao maana kwa sehemu yao walifanya ya kupendeza na mengi yalikuwa na faida kwetu, tuyarudie maana vya kale ni dhahabu.

Mwenye kuelewa kaelewa.

NHIF yakanusha taarifa za uzushi mtandaoni
Wazazi watakaoshindwa kuwapeleka Watoto shule kukiona