Wakati fulani niliwahi kukutana na Mwalimu wangu, rafiki yangu na Mkufunzi wangu, Doto Bulendu na katika mazungumzo yake ambayo baadaye aliyaweka kimaandishi alisema hana shaka kuwa kwa wale wabobezi ya masuala ya kimataifa watakuwa wanajua kuwa Dunia imeshaondoka kwenye mfumo wa utawala wa mabavu na leo mataifa yanaumiza akili kutawala kwa akili, utamaduni, teknolojia na fikra.

Akasema, utaratibu unaotumika sasa ni kama vile tulivyohama kutoka analog kwenda dijitali yaani wanaachana na ‘Hard Power’ na kuingia kwenye ‘Soft Power’ Mmarekani leo ili akutawale hawezi kuja kwa njia za miaka ya 50 ya kimabavu, yeye anachokifanya ni kuhakikisha utamaduni wake unatawala Dunia kwa teknolojia yake ndiyo maana TikTok ilipigwa marufuku Marekani kwani ilikuwa tishio kwa X (zamani Twitter), ambayo inatawala Dunia.

Mmarekani, ili aitawale Dunia atahakikisha maktaba za Shule mpaka Vyuo Vikuu zimejaa vitabu vilivyoandikwa na Wamarekani, ili mwisho wa siku fikra na akili ya Mmarekani iamue matumizi ya Cheti, Stashahada, Shahada za Dunia nzima.

Wajerumani wanapokuja Afrika na kuweka pesa Kwenye Miradi ya maendeleo hapo nia ni kujenga himaya yao na hiyo kwenye masuala ya kimataifa tunaita “Soft Power” ambapo na hata  Mchina anapohakikisha Dunia nzima inatumia Wechart badala ya Whatsapp, TikTok badala ya X, Dingtok badala ya Zoom hiyo tunaitwa “soft power strategy”.

Muingereza anapohakikisha Dunia nzima inakitumia Kingereza kwenye shughuli rasmi na siyo Kiswahili, Kireno, Kifaransa wala Kijerumani hiyo ndiyo “soft power strategy”.

Mtazame Mchina anavyopambania Kichina kizungumzwe Duniani, mtazame anavyosomesha mamia kwa maelfu ya Vijana tena wakifundishwa utamaduni na fikra za wanazuoni wa Kichina na siyo Wamarekani, hiyo kwenye mahusiano ya kimataifa inaitwa “Soft power strategy”.

Tazama Walimu Na Wakufunzi kutoka Ulaya, Marekani na Asia wanavyoingia Afrika kufundisha mashuleni mpaka Vyuo Vikuu Kwa kujitolea, hiyo ndiyo “Soft power strategy” na ndipo Dunia ilipo na inapoelekea.

Leo Wajapani, Wachina, Waturuki wanapishana barani Afrika kujenga Miundo mbinu mikubwa huku wakiweka kumbukumbu sawa kuwa Miradi hiyo imejengwa kwa hisani yao, hiyo ndiyo “soft power strategy” na Dunia ndipo ilipo.

Kiufupi Afrika inashindwa kimkakati kuchukua sehemu ya utawala wa kipande cha Dunia na ndiyo maana unamkuta Kiongozi Mkubwa wa Kiafrika anasema hatuwezi kutawaliwa ila anaandika Maneno hayo kwa kutumia simu ya Mmarekani.

Aidha, ili aweze kuongeza maarifa na kuandaa somo wakati mwingine anatumia laptop ya Mmarekani, mitandao ya Kijamii anayotumia ni Facebook, X, na Whatsapp halafu anasema hataki kutawaliwa. Dunia haipo kwenye “Hard Power” wala wasidhani eti siku moja watakuja na kuwa Wakuu wa Mikoa au ma DC, hapana Dunia imeshatoka huko.

Unamkuta mtu ni msomi anafundisha darasani kuwa waafrika tusikubali kutawaliwa lakini maudhui anayofundisha ni ya Mmarekani, Projector anayotumia ni ya mchina, Internet anayotumia ni ya Mmarekani.

“Binafsi huwa najiuliza sana hivi mtu anaposema ,sisi ni taifa huru hatuwezi kukubali kutawaliwa huwa ana Maana gani? anajua kweli Dunia inavyotawaliwa Kwa Sasa?,” aliuliza Bulendu.

Anasema, kama kweli tunataka kutoka kwenye makucha ya hao wanaoendelea kukutawala basi ni wakati sasa wa Serikali za Kiafrika kuanza kuwekeza sana kwenye

1. Ugunduzi

2. Sayansi

3. Elimu ya Kiafrika

4. Sera za Kiafrika

5. Je Kama China imetafuta mbadala wa X, Facebook, Zoom na Whatsapp sisi Afrika tuna mpango gani?

6. Wachina waliizuia BBC nchini kwao lakini wakahakikisha Shirika la utangazaji la China lipo kila pande za Afrika likipambana na DW, BBC, RFI na VOA, Je chombo gani cha kutoka Afrika kinapambana na hivyo vyombo vya Habari vinavyotamba Duniani?.

Tunapojadili namna ya kuwa huru tujue “Hard power strategies” hazitumiki sasa ilikuwa ni  wakati wa Mkutano wa Berlin kati ya Desemba 1884 – Feb 1885. Dunia ya leo inatawaliwa na “Soft power strategies” Watu wanatawala kikili, kifikra, kimawazo, kisayansi, kiteknolojia na kiutamaduni.

Wananchi wapewe nafasi kujiamulia hatma yao - Kinana
Wapinzani msiandamane nendeni Mahakamani - Wanaharakati