Licha ya Serikali ya Malawi kupiga marufuku uagizaji wa mahindi ambayo hayajasagwa kutoka Kenya na Tanzania, kwa hofu ya kuenea ugonjwa “Necrosis” wa mahindi, au MLN, nchi hiyo itapokea Unga kutoka Tanzania.
Hatua hiyo inatokana na uhaba wa chakula ulipo katika Taifa hilo, hali ambayo itawasaidia Wamalawi kupata chakula, ambapo shirika la mpango wa chakula duniani – WFP, limeanza kusaga tani 30,000 za mahindi ya msaada.
Kamishna wa Idara ya masuala ya kukabiliana na maafa ya Malawi, Charles Kalemba kuagiza unga ni salama zaidi na kuongeza kuwa, “Tunapata unga wa mahindi kutoka Tanzania kwa sababu wizara ya kilimo haikusema hatuwezi kupata unga. Mahindi ambayo yanaweza kupandwa, ndiyo yenye tatizo. Lakini kupata unga kamili wa mahindi ni sawa.”
Hata hivyo, mkurugenzi wa WFP wa Malawi, Paul Turnbul, aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa kutokana na muda, ilikubaliwa kutofanyika vipimo vyovyote na badala yake WFP itayasaga mahindi na kuingiza unga Malawi.
Malawi inakadiria kuwa watu milioni 4.4 na takriban robo ya wakazi wa Taifa hilo, watakabiliwa na uhaba wa chakula katika kipindi cha miezi mitatu ijayo na uhaba wa chakula unatokana na athari za kimbunga Freddy, ambacho kilisomba maelfu ya hekta za mazao mwaka 2023.
Aidha, Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa akiba ya mahindi katika hifadhi ya kimkakati ya kitaifa imeshuka hadi tani 68,000, kutoka 100,000 chini ya mahitaji ya kukabiliana na njaa katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.