Maana ya maisha ni nini? Nawezaje kupata utimilifu, lengo na kutosheka maishani mwangu? Je, nitafanikiwa kuwa na uwezo wa kutimiza jambo la kudumu? Watu wengi hawajaacha kufikiria juu ya maana ya maisha ni nini.
Binadamu huangalia nyuma na kuhuzunukia uharibifu uliowapata na hata kusahau yale mema waliyofaulu kuwa nayo. Malengo mengi huthibitisha utupu wake baada ya miaka kadhaa kupita yakishughulikiwa.
Katika maisha yetu ya siku baada ya siku, watu hushughulikia malengo mbalimbali wakidhania watapata maana ya maisha ndani yake.
Malengo haya ni kama mafanikio ya kibiashara, mali, uhusiano mzuri, mapenzi, tafrija, kutendea wengine mema, na kadhalika.
Watu wamewahi kushuhudia ya kwamba hata baada ya kufaikiwa katika malengo yao ya mali, uhusiano, raha, kulibaki bado utupu ndani yao pamoja na kutotosheka ambako hakuna kitu kingine kingejaza.
Hii ilinifanya nikumbuke wakati fulani ambapo Mwalimu wangu Dotto Bulendu aliwahi kusema Binadamu anapokuwa kwenye anguko lolote maishani hupitia hatua tano.
Hatua hizo tano ni vipindi ambavyo hutofautiana kwa mtu na mtu ambaye hutegemea na mambo mengi, wengine hatua ya kwanza huchukua hata mwaka.
1. Kukataa.
Hapa husema hapana, haiwezekani, haiwezekani, siyo kweli. Mfano mtu kapata ugonjwa, akiambiwa una maambukizi ya ugonjwa fulani, hukataa.
Wapo watu huingia kwenye anguko la mahusiano ama ndoa, hapa yupo mmoja hukataa kuikubali hali hiyo na kusema haiwezakani na wengine hufanyiana vurugu.
2. Hasira.
Hapa mtu humwambia Mungu, kwa nini mimi?kwa nini siyo wengine.Katika hatua hii mtu huwa mkali kwa kila mtu kuanzia nyumbani mpaka ofisini.
3. Sonona.
Hatua hii ni mbaya yaweza sababisha matatizo makubwa kama kiharusi, shinikizo la damu,n.k.Hasira husabahisha mtu kuchukua uamuzi mgumu, wengine hujaribu hata kuondoa uhai wao,wengine hutaka kulipiza kisasi.
4. Majadiliano.
Mtu huanza kujadiliana na Mungu juu ya kukubali ama kutokukubali juu ya lililomfika.Hapa ndipo watu wa karibu hujitokeza na kumpa maneno ya faraja.
Wengine humpa mifano mingi yenye kushabihiana na tatizo lake ili asijione yeye pekee ndiyo mwenye kuumizwa.
5.Kukubali.
Hii ndiyo hatua ya mwisho kwa mwanadamu, kama alikuwa mgonjwa, husema kwa mateso haya nakubali kufariki.
Hatua hii inapofikia kwa wale Wakristo Yesu aliomba maji akasema “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu,” pia alisema “Baba ikiwezekana kikombe hiki nikiepuke.”
Kiuhalisia yale yanayozungumziwa katika aya hizi ni kwamba bado tuna nafasi ya kuchagua na pia bado tunaweza kuendelea kuyaongoza maisha yetu wenyewe kwa hekima na kwa kuchukua mifano mingine ya watu walioshinda magumu na wakafanikiwa.
Na kutokana na shida au mazonge wanayokutana nayo, baadhibya watu hujipa matumaini kwa misemo, au wakajipa majina ya usugu wa matatizo wakilenga kutafuta faraja au uhimili wa kutopoteza mwelekeo wa maisha.
Miongoni mwa misemeo ni pamoja na baada ya dhiki faraja, ponda mali kufa kwaja, mchumia juani hulia kivulini, maisha ni kubahatisha au majina kama bingwa wa shida, chuma cha reli na wengine huenda mbali zaidi wakajipa na vyeo eti ni “WAZIRI WA DHIKI NA MIPANGO YA GHAFLA.”
Hii yote huonesha ni jinsi gani wameyaishi matatizo na kupambana nayo na wakashinda, au ni namna gani wanatatua mazonge ya nyakati ngumu na wakafanikiwa katika hali ya kustaajabisha, kiasi cha kupelekea wao kujiona makamanda na wenye bahati za mtende lakini uhalisia hakuna ambaye alipambana katika maisha akatoka patupu kila mtu hula kwa jasho lake, mafanikio ni lazima maishani ukijishugulisha na hapo utakuwa umeyapatia maisha.
Kikubwa hapa, tusichoke kupambana, tusichoke kuvumilia magumu na katika maisha usiende na taswira chanya pekee, kuna wakati kukosa kupo, kufeli kupo pia, hakuna shujaa pasipo na mapambano na jambo jema huwa haliji kirahisi, MAISHA NI VILE UNAVYOISHI.