Wakati Dirisha Dogo la usajili likifungwa Usiku wa Kuamkia Leo Jumanne (Januari 16), wachezaji 24 wamesajiliwa na kutambulishwa katika baadhi ya timu za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wachezaji hao wamesajiliwa kupitia Dirisha Dogo kwa lengo la kuziongezea nguvu timu zilizowasajili.
Katika usajili huo, klabu ya Mashujaa FC ya Kigoma, imeongoza kwa kusajili wachezaji wanane huku Simba ikinasa huduma ya wachezaji wanne na Azam FC imesajili wachezaji watatu wakati Young Africans hadi kufikia jana Jumatatu (Januari 15) jioni, haikuwa imemtambulisha mchezaji yoyote.
Wachezaji waliosajiliwa na Simba SC ni kiungo mkabaji kutoka US Monastir ya Tunisi, Babacar Sarr, Ladack Chasambi aliyetokea Mtibwa Sugar, mshambuliaji kutoka JKU ya Zanzibar, Salehe Karabaka, washambuliaji wa kimataifa Pa Omar Jobe (Gambia) aliyetoka FC Zhenis ya Kazakhstan na Freddy Michael Kouablan (Ivory Coast) aliyetokea Green Eagles ya Zambia.
Azam FC imewasajili kipa Mohamed Mustafa kutoka El Merreikh, Yeison Fuentes na Franklin Navarro wote kutoka Colombia.
Mashujaa imewatambulisha David Ulomi kutoka Afrika Kusini, Ibrahim Ame (KMC), Reliant Lusajo (Namungo), Ibrahim Mussa (Ruvu Shooting), Nyenyezi Juma (Inter Star ya nchini Burundi), Mapinduzi Balama (Mtibwa Sugar), Emmanuel Mtumbuka (Stand United) na mlinda mlango Erick Johora kutoka Geita Gold.
Klabu ya Mtibwa Sugar imepata saini ya Nasoro Kapama na Jimmyson Mwanuke walioachwa kutoka Simba huku KMC ikinasa saini ya Shabani Chilunda, Abdallah Hamis kutoka Simba SC na Abdalah Saidi kutoka Mlandege FC.
Pamoja na klabu hizo, Tanzania Prisons wao imewasajili Abdulkareem Segeja, Ally Msengi na Feisal Mfuko huku Dodoma Jiji ikimtambulisha mchezaji Apollo Onyango kutoka KCB ya Kenya.
Wakati huo huo, tetesi zinaeleza kuwa klabu ya Ihefu FC imenasa saini za wachezaji sita kutoka Singida Fountain Gate ambao ni Marouf Tchakei, Bruno Gomes, Joash Onyango, Elvis Rupia, Duke Abuya na Aboubakari Khomeini.
Wachezaji hao waliosajiliwa kupitia dirisha dogo wataanza kuzitumikia timu zao mpya ligi itakapoendelea baada ya kusimama kupisha fainali za Mataifa Afrika ‘AFCON 20232’, inayoendelea nchini Ivory Coast.