Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi wa Misri, Assem Elgazzar ambapo kikao hicho kilijikita kuzungumzia maendeleo ya mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao kwa sasa umefikia asilimia 95.83.

Mazungumzo hayo yamefanyika hii leo Januari 21, 2024 jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri wa Misri aliongozana na watendaji wakuu wa kampuni ya JV Elsewedy na Arab Contractors (wanaotekeleza mradi wa JNHPP) na kwa upande wa Tanzania, viongozi waliohudhuria ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.

Dkt.Biteko ameeleza kuridhishwa kwake na kazi kubwa inayofanywa na Wakandarasi pamoja na TANESCO huku akieleza kufurahishwa kwake na taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais wa kampuni ya Elsewedy, Eng. Wael Hamdy ya kuwa majaribio ya mtambo namba 9 katika mradi wa JNHPP yameleta mafanikio na kilowati 100 zimeanza kuingizwa gridi ya Taifa.

“Kikao hiki kimejikita kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusu mradi wa JNHPP, Mhe. Waziri Elgazzar ametumwa na Rais wa Misri kwa ajili ya kuona maendeleo ya mradi huu, jambo lililotufurahisha hapa ni majaribio ya mtambo namba Tisa yanaendelea na kwa hatua ya mwanzo ambayo wamejaribu kuzungusha mtambo kwa njia ya maji wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na wameingiza kilowati 100 kwenye gridi ya Taifa.” Amesema Dkt. Biteko

Amesema, mafanikio ya majaribio hayo yanaleta matumaini kwani ratiba ya kazi inaenda mapema zaidi ya iliyopangwa mwanzo na hii ni kutokana na kazi nzuri ya Wakandarasi pamoja na TANESCO na kwamba lengo ni kuzalisha megawati 235 kutoka mtambo namba 9 ifikapo Februari mwaka huu na kuendelea na mitambo mingine ikiwemo mtambo Namba 8 na Namba 7.

Ameongeza kuwa, mradi huo ni wa kipaumbele cha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ili watanzania wapate umeme wa uhakika kwa kuwa mradi huo ukimalizika utaingiza megawati 2115 katika gridi ya Taifa.

Amesema kuwa, katika kikao hicho wamezungumza pia kuhusu masuala fedha zilizotengwa kwa ajili ya huduma za kijamii zinazotokana na uwepo wa mradi huo ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya mkataba.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameomba Watanzania wawe na subira wakati Serikali ikitekeleza miradi mbalimbali itakayoongeza kiasi cha umeme nchini ikiwemo mradi huo wa JNHPP.

Vilevile amesema kuwa, mradi wa JNHPP ni wa kielelezo kwa Afrika kwani inaonesha kuwa nchi za Kiafrika zinaweza zenyewe kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi wa Misri, Mhe. Assim Elgazzar amesema kuwa nia ya Serikali hiyo kutoka mwanzo ni kuona kuwa mradi huo unakamilika kwa ufanisi na kwa wakati na amewapongeza wakandarasi pamoja na TANESCO kwa hatua nzuri ya utekelezaji wa mradi huo.

Amesema kuwa, Serikali ya nchi hiyo itaendelea kuwapa ushirikiano Wakandarasi hao katika hatua zote za utekelezaji wa mradi na kueleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa kwa kampuni za nchi hizo kuendelea kuaminika kwenye utekelezaji wa miradi mingie ikiwemo ya umeme.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Tuzo ya Malkia yamfikisha Prudencia kwa Watoto
Viongozi Wakuu China, Poland, Cuba kutembelea Tanzania