Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameeleza kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona viongozi wote wanatatua kero na changamoto za wananchi na kwamba anasikitishwa na baadhi ya viongozi ambao hawatatui changamoto za wananchi mpaka pale anapofanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini.

Dkt. Biteko amesema hayo hii leo Januari 25, 2024 wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Magodi na Kigandini wilayani Mkinga mkoani Tanga mara baada ya kuwasha umeme katika vijiji hivyo ambao umesambazwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Katika ziara yake kwenye Vijiji hivyo, aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba, Mbunge wa Mkinga ambaye ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Amesema, “Mhe. Rais anafanya kazi kubwa katika kila Sekta na mabilioni ya pesa yamekuwa yakipelekwa kila Mkoa kwa ajili ya kuboresha huduma za wananchi, nikitolea mfano hapa Tanga Serikali ya Awamu ya Sita imeshaleta shilingi Trilioni 2 na Bilioni 600 kwa ajili ya miradi ya maendeleo”

“Kwenye umeme miradi inaongezeka kwani mmepata bilioni 133.6 huku Wilaya ya Mkinga ikipata bilioni Nane kwa ajili ya usambazaji umeme, Dkt. Samia anapambana ili kuwaletea maisha bora watanzania hivyo viongozi wengine tusiishie kusikiliza kero tu bali tuzitatue na kama kuna mahali tunahitaji watupe muda, tuwaambie kwa uwazi,” alisema Biteko.

Katika hatua nyigine, Dkt. Biteko amewataka Wazazi na Walezi nchini kupeleka Shule watoto wote wanaostahili kuwa mashuleni katika kipindi hiki ambacho Shule zimefunguliwa ili wapate elimu itakayowasaidia katika maisha yao na nchi kwa ujumla, akitolea mfano kwa Mkoa wa Tanga watoto walioripoti Shule ni asilimia 60.

Wanafunzi wanusurika kifo kwa radi Morogoro
Mvua zazuia biashara Moro, Wananchi wavunja ukimya