Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wanaoishi katika maeneo hatarishi hasa ya mabondeni, kuondoka ili kupunguza maafa yanayoweza kusababishwa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kishapu, Boniphace Butondo katika kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, aliyetaka kufahamu Serikali imejipangaje kibajeti kurudisha miundombinu iliyoharibika kutokana na mvua.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu pia amewataka watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania – TANROADS na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wahakikishe wanafuatilia maeneo yaliyoathirika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na wafanye ukarabati wa kurejesha miundombinu iliyoharibika zikiwemo barabara na madaraja.
Hata hivyo, Majaliwa pia ametumia fursa hiyo kuwahakikishia Wananchi kuwa Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha inarejesha miundombinu iliyoharibika kutokana na mvua hizo inarudishwa ili wananchi waendelee na shughuli zao.