Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaasa wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa familia na Taifa.
Mchengerwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Ikwiriri kwa njia ya video akihitimisha Kampeni Uhamasishaji na utoaji wa Elimu, huduma za Afya na Chanjo katika kipindi cha AFCON 2023.
Amesema serikali imewekeza katika sekta ya Afya na inaendelea kuboresha huduma za Afya kwa kusogeza miundombinu ya kutolea huduma,upatikanaji wa vifaa tiba na watoa huduma kuanzia ngazi ya Zahanati,Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya.
“Tumefanikisha mambo mengi yanayorahisisha utolewaji wa huduma katika sekta ya Afya ili kuleta Faraja kwa kusogeza huduma kwa wananchi kwa ujenzi wa Hospitali,vituo vya Afya,ujenzi wa zahanati na uletaji wa vifaa tiba hasa katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya sita, ili serikali iendelee kufanya vizuri inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele amewaomba wananchi wa Rufiji kuchangamkia fursa zinazojitokeza ikiwemo ya huduma za uchunguzi wa Afya na chanjo bure kwa ajili ya kukinga familia zao na magonjwa mbalimbali ikiwemo ya mlipuko.