Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi – CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema watu wanaweza kupishana katika maelezo ya kumwelezea Hayati Edward Lowassa katika mambo mbalimbali, lakini hawezi kubishaniwa kama mchakapakazi wa kweli, katika kuwatumikia Watanzania.
Dkt. Nchimbi amesema kupitia uhodari wake wa kuchapa kazi katika kutimiza wajibu wake kwa nchi, Hayati Lowassa alikuwa kiongozi mwenye uthubutu na uwezo wa kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya kutafuta ufanisi na kupata matokeo chanya ya haraka kwa ajili ya maendeleo ya watu.
Dkt. Balozi Nchimbi ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari, baada ya kufika kuwapatia pole wafiwa, kusaini kitabu cha maombolezo na kutoa heshima za mwisho, nyumbani kwa Hayati Lowassa, katika Kijiji cha Ngarash, Wilayani Monduli Mkoa wa Arusha.
Amesema, “Lowassa alikuwa mchapakazi kweli kweli. Alikuwa mtu wa maamuzi magumu. Watu wanaweza wakapishana katika kila maelezo wanayotoa kuhusu Lowassa lakini hakuna hata mtu mmoja anayeweza kuwa na ujasiri wa kusema alikuwa mvivu, au alikuwa hapendi kufanya kazi au hakuwa na mapenzi na nchi yake, hakuna.”
“Alikuwa mzalendo, mnyenyekevu na aliyependa watu wote bila kuwabagua. Moja ya uamuzi mgumu unaoendelea kukumbukwa ni hatua ya kiongozi huyo aliyoichukua ya kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008,” ameongeza Dkt. Nchimbi.