Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema ana siku kumi ngumu kwenye mechi nne za ligi zilizo mbele yao huku akisisitiza kuwa kila mchezaji ana nafasi ya kucheza kwenye mechi hizo.

Gamondi amesema ana mechi nne ndani ya siku kumi, mechi mbili atacheza nyumbani na mbili ugenini, lakini kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji wake kwa kuhakikisha wanatinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, na kila sababu ya kuwatumia nyota wote wa kikosi hicho kwenye mechi hizo nne ili kujenga usawa na uimara wa timu.

Amesema kuwa kubana kwa ratiba ya Ligi Kuu kunamlazimisha kutoa nafasi kwa kundi kubwa la wachezaji kama njia ya kuepuka uchovu wa kikosi, ambao unaweza kuchangia wasifanye vizuri huku akisisitiza kuwa ratiba ya Robo Fainali pia ipo karibu.

CAF inatarajiwa kutangaza wakati wowote siku ya upangwaji wa droo ya mechi za kuanzia hatua ya Robo Fainali hadi Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans inatarajia kuanza na Namungo FC ugenini ljumaa hii na baadae kurudi kuikabili Ihefu FC Machi 11, Geita Gold Machi 14 na kumaliza na Azam FC Machi 17 hivyo inalazimika kucheza mechi nne ndani ya siku 10 ikiwa na maana ya kuwa na siku tatu tu za kujiandaa kutoka mechi moja hadi nyingine.

Mrundikano huo wa mechi kwenye ratiba umetokana na viporo ambavyo Young Africans na Simba SC wamekuwa navyo kutokana na kusogezwa mbele kwa baadhi ya mechi zao ili kuzipa nafasi timu hizo kujiandaa na kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Akizungumzia ugumu huo wa ratiba ulio mbele yake, Gamondi amesema kuwa namna pekee ya kukabiliana nao ni kufanya mabadiliko ya mara kwa mara ya vikosi ili kutochosha wachezaji ambao wana kibarua cha kutetea mataji na kusaka historia zaidi kwenye michuano ya CAF.

“Najivunia wachezaji wangu wote kuwa kwenye ushindani na wamekuwa wakihitaji nafasi ya kucheza ili kuipambania timu, hivyo naamini nafasi nitakazotoa wachezaji hawataniangusha.”

“Kutokana na ugumu wa ratiba natarajia kufanya mabadiliko makubwa ya mara kwa mara kwenye kikosi ili kutoa nafasi ya wachezaji wengine kukusanya nguvu mpya huku wengine wakipambania timu kufikia malengo”

“Nina imani kubwa na wachezaji waliopo kikosini naamini kila mmoja atafanya kazi yake kwa usahihi akipata nafasi ya kucheza, lengo ni moja kukusanya pointi zitakazotufanya tutetee ubingwa.

Benchikha anazitaka zote 12
Zuchu marufuku Zanzibar