Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amemuelekeza Naibu Katibu Mkuu, Sekta ya Mifugo, Prof. Daniel Mushi kuhakikisha anawawezesha Vijana wa kikundi cha Kanani Msomera, walionzisha wao wenyewe programu ya BBT kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kuunga mkono dhamira ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwainua Vijana kiuchumi kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT).

Waziri Ulega ametoa maelekezo hayo mapema wiki hii, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya mifugo inayotekelezwa katika Kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni, mkoani Tanga ambapo aliwatembelea vijana hao ambao wameanzisha programu yao ya kunenepesha mifugo na kuiuza.

Alisema, “ninyi hamkutaka kusubiri, mmeona programu ya Mhe, Rais Samia ya BBT na mkasema hapa Msomera mnaanzisha BBT yenu, hongereni sana, sasa natoa maelekezo kwa Naibu Katibu Mkuu kuwaangalia kwa ukaribu vijana hawa walioanzisha BBT wao wenyewe kuhakikisha wanapewa kipaumbele katika elimu ya ufugaji na mitaji kwa kuwaunganisha na Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) ili wapatiwe mikopo nafuu isiyokuwa na riba.”

Waziri Ulega aliongeza kuwa Vijana wameunga juhudi zaRais kwa vitendo bila kusubiri na hivyo ni lazima waungwe mkono ambapo aliwakabidhi Mbegu za Malisho na Mbuzi 10 waliotolewa na Shirika la Heifer International kama ruzuku, ikiwa ni sehemu ya kuwatia chachu katika jitihada zao.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Heifer International, Mark Tsoxo amesema kuwa wao tayari wameshirikiana na kikundi hicho cha vijana na wameshawapatia elimu juu ya biashara, masoko na uendeshaji wa vikundi, huku pia wakiwapatia mbuzi vijana hao ambao wameona ndoto ya Mhe, Rais ya kuwainua vijana kupitia program ya BBT.

RC Malima: Tokeni mkaseme vitendo vya ukatili dhidi ya Watoto
TPF-Net Arusha wawagusa Watoto wa Askari waliofariki ajalini