Boniface Gideon – Tanga.

Wajumbe wa Kamati ya Washauri Mkoa wa Tanga, wamejadili hoja mbalimbali ikiwemo miundombinu ya Barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara Nchini – TANROAD na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini – TARULA, huku wakitaka kasi ya ujenzi kuongezwa kwa baadhi ya maeneo ikiwemo Barabara ya Tanga- Pangani, Handeni -Kilindi na Daraja la Pangani.

Aidha, wajumbe hao pia wamepitisha ombi la Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 ya Bil.415 kwaajili ya matumizi ya mwaka mkoa wa Tanga.

Mbunge wa Jimbo la Handeni Vijijini, John Sallu ambaye aliongoza kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, ilizipongeza Mamlaka zinazosimamia ujenzi wa miundombinu ya Barabara TARULA na TANROAD kwa kuwezesha maeneo mengi ya Mkoa wa Tanga kupitika muda wote,

Amesema, “TANROAD na TARURA mmejitahidi sana kwakutuboreshea miundombinu ya Barabara nyingi zinapitika,lakini tunaomba muongeze kasi kwenye baadhi ya maeneo, tunataka Barabara ya Handeni-Kilindi mpaka mikoa ya jirani ikamilike kwa haraka ,lakini pia Barabara ya Tanga-Pangani pamoja na ujenzi wa Daraja kubwa pale Pangani ,kasi bado hairidhishi.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Akida Bahorera alizitaka TANROAD na TARURA kuhakikisha wanamalizia Barabara zote kabla ya mwaka 2025, ili kupunguza maswali ya Wananchi,

“Tunaomba mmalizie Barabara zote hasa zile ambazo mlizianza, Barabara ya Tanga-Pangani na Daraja kubwa pale Pangani bado hatufurahishwi kiukweli,tunazo Barabara za Vijijini nazo tuziangalie mana tunaenda kwenye mvua za masika,” alisema Akida.

Naye Mwenyekiti wa Halmshauri ya Korogwe Mji, Francis Komba alisema licha ya Barabara nyingi kupitika lakini bado kuna maeneo yanatakiwa kuwekwa madaraja Makubwa kabla ya mvua za masika hazijaanza kunyesha.

“Mvua za Masika zitaanza wakati wowote kuanzia sasa na tunatakiwa tuchukue tahadhari ili yasije yakatokea ya wenzetu, kwahiyo hakikisheni mnaweka madaraja Makubwa ili Maji yapite bila kikwazo kuepusha mafuriko” Alisema Komba.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 11, 2024
Dkt. Biteko: Rais Samia hataki misukosuko kwa Wafanyabiashara