Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imesema mojawapo ya siri iliyouwezesha mgodi huo kuongoza nchini kwa kuongeza idadi kubwa ya Wanawake walioajiriwa kwenye sekta hiyo ya madini, ni kubuni na kutekeleza kwa vitendo sera na miongozo inayohamasisha usawa wa kijinsia maeneo ya kazi.
Hayo yamebinishwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Makamu Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayeshughulikia miradi endelevu na masuala ya ushirika Afrika, Simon Shayo katika sherehe za awali za kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Amesema hivi sasa asilimia 13 ya nguvukazi ya kampuni hiyo ni wanawake ilihali kwa upande wa kimataifa ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini takwimu zinaonesha ni kati ya asilimia 14 na 16.
“Kwa hivyo hatufanyi vibaya. Tuliendesha mgodi bila uwepo wa wanawake katika nafasi za juu za uongozi lakini sasa wapo na wengine wamevuka mipaka na kwenda kuwa wasimamizi wa sekta hiyo katika kampuni mbalimbali nje ya nchi,” alisema.
Alisema sera na miongozo ya GGML iliyowekwa sio kwamba imeongeza idadi ya wanawake kushiriki kwenye shughuli za mgodi huo, bali pia hata kubadilisha hulka za wanaume waliopo kwenye kampuni hiyo na kuona umuhimu wa wanawake kuwepo kwenye sekta ya madini.
Shayo alitaja baadhi ya miongozo hiyo kuwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuajiri ambao unatoa kipaumbele kwa wanawake.
“Katika ajira asilimia 50 ni wanawake na asilimia inayobaki 50 ni wanaume na kama watalingana ufaulu katika usaili anayepewa kipaumbele ni mwanamke,” alisema.
Alisema pia kampuni hiyo hutoa ufadhili kwa wafanyakazi wake wanawake kwenda kupata mafunzo ya juu ya uongozi yanayotolewa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ambapo tangu mafunzo hayo yaliyopewa jina la Female Future Program (FFT), yaanze mwaka 2016, wanawake 23 kutoka GGML wamefadhiliwa na kuhitimu mafunzo hayo.
“Pia ndani ya mgodi tuna muongoo unaoitwa ‘don’t cross the line’, kwamba usivuke mpaka au mstari kwenda kumghasi, kumtendea ukatili wowote mwanamke na kama kukitokea jambo lolote kuna namba za simu za kutoa taarifa kwa njia ya siri na hatua kuchukuliwa,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye hafla hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa alisema kampuni za madini zinatakiwa kuzingatia kanuni ya ‘Local Content’ iliyopo kwenye mabadiliko ya sheria ya madini kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wanawake kwenye masuala ya ununuzi.
Alisema kipengele hicho cha ushirikisha wazawa katika mnyororo wa thamani, pia ni fursa nzuri kwa kampuni za madini kushirikisha wanawake katika manunuzi mbalimbali ambayo yanatengewa bajeti kubwa kuliko hata kodi zinazolipwa kwa serikali.
“Wanawake wanaojishughulisha kwenye shughuli za sekta ya madini wamekuwa na mchango mkubwa katika kujenga uchumi wao na pato la Taifa,” alisema Slaa.