Licha ya kuongoza katika msimamo, Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Angel Gamondi, amesema vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara bado ni ngumu na ana wasiwasi wa kupata pointi zote sita kutoka kwa Simba SC na Azam FC.
Young Africans inajiandaa kukutana na Azam FC keshokutwa Jumapili (Machi 17) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Akizungumza jijini humo, Gamondi amewakata wachezaji wake kupambana kuvuna pointi tatu katika kila mechi watakayocheza kuanzia mchezo dhidi ya Azam FC ili kuhakikisha wanaendelea kujiimarisha kileleni na kujiweka kwenye nafasi nzuri za kuwania ubingwa.
Gamondi amesema licha ya kuongoza ligi lakini bado ana michezo mingine migumu iliyopo katika hatua za lala salama na imetokana na wapinzani wao kujiimarisha.
Kocha huyo amesema ili kujiweka salama wanatakiwa kuvuna pointi tatu katika kila mechi kwa ajili ya kujiweka kwenye mazingira mazuri na kwao wanaheshimu kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Bado sina uhakika wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu licha ya timu yangu kuendelea kupata alama tatu katika kila mechi tunayocheza, naendelea kukiandaa kimbinu kikosi changu ili kizidi kunipatia matokeo kila mchezo ukiwamo dhidi ya Azam FC, Simba SC pamoja na michezo yote iliyopo mbele yetu,” Gamondi amesema.
Ameongeza bado joto la ligi linaendelea kupanda na hajiaminishi moja kwa moja ana uhakika wa kushinda taji hilo.
“Licha ya kupata Ushindi na kufunga mabao mengi katika kila mechi, kila mchezo tunaendelea kukutana na timu zinazotupa ushindani katika mzunguuko huu wa pili,” ameongeza kocha huyo kutoka nchini Argentina.
Gamondi amesema kulingana na ugumu wa ligi hiyo hataidharau timu yoyote na kutoangalia udogo wa wapinzani wao, zaidi ya kutafuta pointi tatu zitakazowapeleka kufikia malengo yao.
“Tunatakiwa kupambana, wachezaji wajitume zaidi, hatuwezi kuridhika kwa kuwa tunaongoza ligi kwa alama kumi ambazo ni ndogo sana katika mchezo wa mpira wa miguu,” amesema Gamondi.
Young Africans inaongoza ligi ikiwa na pointi 52 na keshokutwa Jumapili (Machi 17) watakutana na Azam FC iliyoko katika nafasi ya pili ikiwa na alama 44 kibindoni, lakini imecheza michezo miwili zaidi. Wekundu wa Msimbazi ambao baadae leo Ijumaa (Machi 15) wataikaribisha Mashujaa wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 42, lakini wamecheza michezo 18.