Klabu ya Simba SC Tanzania na Al Hilal SC ya Sudan zimetuma ofa Azam FC ili kuhitaji huduma ya Mshambuliaji kutoka Zimbabwe Prince Dube.

Dube tayari ameshadhihirisha nia yake ya kuondoka Azam FC kufuatia kuwasilisha barua ya kuvunja mkataba mwanzoni mwa mwezi huu, na kwa sasa hayupo kwenye kikosi cha klabu hiyo yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam.

Azam FC imethibitisha kutumwa kwa ofa za klabu hizo mbili kupitia taarifa maalum iliyochapishwa katika vyanzo vya habari vya klabu hiyo, huku ikizitaka klabu nyingine zenye nia ya kuhitaji huduma ya Mshambuliami huyo kutuma ofa zao.

“Azam FC inathibitisha kwamba imepokea ofa kutoka vilabu viwili tofauti vikimhitaji mchezaji wetu, Prince Dube, raia wa Zimbabwe.

“Ofa hizo zimetoka katika vilabu vya Simba SC ya Tanzania na Al Hilal SC ya Sudan. Uongozi unazifanyia tathmini ofa hizo ili kuona ipi inafaa.

“Aidha, Azam FC inavikaribisha vilabu vingine kuleta ofa zao kwani milango bado iko wazi.” Imeeleza taarifa iliyotolewa na Menejimenti, Azam Football Club, Machi 14, 2024.

Awali Young Africans ilikuwa ikitajwa kumuhitaji Mshambuliaji huyo, lakini ukimya wake hadi sasa, una maanisha huenda ilikuwa inahusishwa ndivyo sivyo.

Nani kupangwa na nani UEFA CL?
Mbaroni kwa mauwaji ya watatu akiwemo Mama yake