Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro, ametoa maagizo kwa uongozi wa Chama Cha Netiboli Tanzania (CHANETA), kuendeleza programu muhimu za mchezo huo ikiwemo kung’amua vipaji.

Ndumbaro ametoa maagizo hayo, alipokutana na uongozi wa CHANETA katika ofisi za chama hicho zilizopo Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Dk. Ndumbaro amesema, CHANETA inapswa kuendeleza programu muhimu ambazo zitaongeza vipaji ya vijana nchini.

Amefafanua kuwa ana imani kupitia mashindano ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) na Michezo kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) kutapatikana vipaji vingi.

“Viongozi mliopo kwa maslahi ya mchezo wa Netiboli Tanzania, si vyema mkaendekeza sana migogoro katika chama, bali mnapaswa kuendeleza programu muhimu zilizopo ikiwemo kung’amua vipaji kutoka mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA” amesema.

Hata hivyo, katika kikao hicho, Dk. Ndumbaro ameutaka uongozi huo kutoendekeza migogoro katika chama, bali kuwa na umoja na mshikamano kwa maslahi ya mchezo wa Netiboli nchini.

“Mnapaswa kuachana na migogoro ambayo haina faida katika mchezo huu, mnatakiwa kushirikiana na kuwa na umoja ambao utawasaidia kupiga hatua Netiboli, pamoja na kusimamia vizuri maandalizi ya timu ya taifa iweze kufanya vyema mashindano ya kimataifa,” amesema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa CHANETA Dk. Devotha Marwa ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na serikali kwa uongozi huo, pamoja na kuendelea kukiongoza chama kwa weledi zaidi.

“Nitahakikisha nafuata maagizo niliyopewa na serikali mimi na mwenzangu, tutahakikisha tunazingatia kwa lengo la mchezo huu kupiga hatua na kuacha historia katika mashindano ya kimataifa.” amesema

Sebastien Haller kuwakosa Benin, Uruguay
Usiyoyajua kwa Mohamed Salah