Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Prof. Paramagamba Kabudi amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya Shule katika Kijiji cha Kitange mbili kilichopo Kata ya Mtumbatu Wilaya Kilosa mkoani Morogoro na kutembelea Shule ya Sekondari ya Kitange, ambayo ujenzi wake unaendelea huku akiwataka Wazazi kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shule.

Kauli ya Prof. Kabudi inakuja baada ya kugundua kuwa idadi ya wanafunzi Walioripoti Shuleni ni ndogo ikilinganishwa na idadi iliyopangwa huku Shule hiyo ambayo ujenzi wake ulianza mwaka 2022 hadi sasa imepata msaada kutoka kwa Serikali na wadau mbalimbali, ili kuiwezesha kutoa fursa bora za elimu kwa Wanafunzi wa eneo hilo.

Mkuu wa shule, Cecilia Chipeta amearifu maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo akisema bado kuna ambao hawajaripoti na hadi sasa ni Wanafunzi 84 pekee kati ya wanafunzi 198 walioripoti, huku Katibu wa Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilayani Kilosa, Selina Shayo akionyesha kusikitishwa na hali hiyio na kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa jamii.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mtumbatu, Amani Sewando ameahidi kushirikiana na viongozi wa kijiji kutafuta wanafunzi ambao bado hawajajiunga na shule ambapo Prof. Kabudi pia akatembelea ujenzi wa shule ya sekondari ya Dumila na kukagua maendeleo ya ujenzi na kusisitiza jinsi Serikali ilivyojitoa kuboresha miundombinu ya elimu.

Hata hivyo Ujenzi huo unaogharimu kiasi cha shilingi milioni 125, unaendelea kwa ufanisi na kutoa matumaini ya fursa bora za elimu kwa Wanafunzi wa eneo hilo.

Nishati safi ya kupikia: Wizara kuanzisha Kitengo maalum
Wasiotambulika wavamia, kuiba vifaa vya misaada