Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Biteko ameagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati kuanzisha Kitengo maalum cha usimamizi wa Nishati Safi ya Kupikia ili kutekeleza kwa ufanisi ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia na siyo tu kuishia kwenye kuandaa na kushiriki makongamano kisha masuala yote yanaishia hapo.

Dkt. Biteko ameyasema hayo hii leo Machi 18, 2024 jijini Mwanza, wakati akifungua Mkutano wa Tano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Nishati wenye lengo mahsusi la kupitia na kupitisha rasimu ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/2025.

Amesema, “Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye kinara wa utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia Afrika hivyo wizara lazima iweke mkakati wa kitaasisi na kimfumo ili kufanikisha ajenda hiyo ili utekelezaji wa suala hili usiwe ni jambo la zimamoto.” Amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amesema Wizara ya Nishati ina jukumu la kuihamisha nchi kutoka matumizi ya mafuta na kuhamia kwenye matumizi ya gesi (CNG) kwa kutengeneza mazingira ambayo yatapunguza utegemezi wa mafuta na hivyo kufanya nchi kujiendesha kwa kutumia CNG hivyo, ameagiza Watendaji wa Wizara kusimamia pia utekelezaji wa suala hilo.

Kuhusu Watumishi wa Wizara ya Nishati, Dkt. Biteko amewakumbusha Watumishi kufanya kazi kwa bidii huku wizara ikiangalia stahiki zao ikiwemo motisha na kuongeza kuwa Watumishi wa Wizara ya Nishati wana deni la kuwatumikia Watanzania kwani ndio waliopewa dhamana ya kusimamia Sekta ya Nishati kwa niaba yao hivyo watimize wajibu huo.

Aidha, ametoa wito kwa Wizara ya Nishati kuwa na utaratibu wa kuwapa motisha watumishi wanaofanya vizuri katika kazi na wale wazembe na wasiotumikia wananchi kwa weledi na kwa wakati watambuliwe pia na kuchukuliwa hatua stahiki.

Hata hivyo, ametoa angalizo kwa wenye mamlaka ndani ya Wizara na Taasisi zake kutoona fahari ya kutumia vyeo vyao kwa ajili ya kuabudiwa na kutukuzwa kwani nafasi walizonazo ni za muda tu, hivyo wajijengee marafiki zaidi kuliko maadui na kujikita katika kuhudumia wananchi na hivyo kuepuka kuchafua utendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 19, 2024
Prof. Kabudi asisitiza umuhimu wa Elimu Kilosa