Scolastica Msewa – Rufiji.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega ameongoza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kutoa msaada wa vyakula tani nne yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5 na boti itakayosaidia usafiri na shughuli za kipindi cha mafuriko kwa waathirika wa Kibiti na Rufiji.

Akizungumza kwa niaba ya Wananchi wa Wilaya ya Mkuranga wakati alipofika kutembelea na kukagua athari za mafuriko ya Wilaya ya Rufiji, Ulega alisema msaada huo ni kwa waathirika Kata 17 za Wilaya hizo.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wamewiwa waende wakawashike mkono kwa chakula hicho cha tani nne za unga wa sembe na dona na mafuta ya kupikia ilikuwanusuru waathirika hao wa mafuriko ya Wilaya za Kibiti na Rufiji.

“Mimi na wenzangu tumejipanga kukabithi boti itakayosaidia shughuli za uokozi na usambazaji wa chakula na huduma kwa waathirika hao wa mafuriko ya Wilaya za Kibiti na Rufiji” alisema Mheshimiwa Ulega.

Akipokea msaada huo, Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amewashukuru Viongozi hao na kusema kiongozi Bora ni yule anayejali Wananchi wakati wa shida zao na kutafuta utatuzi.

Aidha, Mchengerwa pia amekabidhi ahadi yake ya shillingi milioni 50 kwa Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele kwa ajili ya kununua mbegu za kilimo kwa Waathirika wa mafuriko hayo.

Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ameshukuru kwa misaada mbalimbali inayoendelea kutolewa na kuahidi kusimamia misaada hiyo iwafikie walengwa.

Vyombo vya Habari kutotangaza, kuchapisha habari za siasa
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Aprili 12, 2024