EDWARD MORINGE SOKOINE – (Agosti 1, 1938 – April 12, 1984)

April 12 ya kila mwaka Tanzania imekuwa ikifanya kumbukizi ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine aliyefariki Dunia kwa ajali ya gari, na katika wiki hii, Ijumaa Aprili 12, 2024, ndiyo siku ambayo tunaadhimisha miaka 40 ya kumbukizi hiyo.

Edward Moringe Sokoine ni mmoja wa viongozi bora kuwahi kutokea nchini, alifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Dakawa Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro ambapo hapo iliwekwa siku ya kumbukizi kutokana na hadhi yake.

KUZALIWA.

Agosti 1, 1938 katika Kitongoji cha Kilasho kilichopo Jijiji cha Emairete, Monduli Juu mkoani Arusha, Sokoine Ole Severe na Mkewe Napelel Sinyai Noomayaki walipata mtoto wa Kiume,      ambaye ndiye Edward Moringe Sokoine.

Kati ya mwa 1949 na 1953 Edward Moringe Sokoine alisoma Shule ya Msingi Monduli na kisha akajiunga na Monduli Middle School kunzia mwaka 1953 hadi 1956, ambapo mwaka 1956 alijiunga na shule ya Sekondari ya Umbwe baada ya kufaulu vema mtihani wa kuhitimu ‘midle school’.

SIASA.

Januari 1,1961, Edward Moringe Sokoine alijiunga na chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ikiwa ni miezi michache kabla Tanganyika haijapata Uhuru ambapo mwaka 1962, alienda Ujerumani Magharibi kusomea mambo ya Utawala na kurejea mwaka 1963 na baada ya kurejea toka huko alipangiwa kazi kama District Executive Officer (DEO) wa Masai.

Septemba 30, 1965, akiwa kijana mdogo tu wa miaka 27 lakini mwenye akili na ubunifu mkubwa, aligombea Ubunge jimbo la Masai na kumshinda Mpinzani wake Edwarf Carli Boniface Ole Mbarnote aliyekuwa Chifu wa Wamasai. Sokoine alijizolea kura 6,977, Chifu Mbarnote akiambulia kura 871.

Akiwa Bungeni baada tu ya kuapishwa Bungeni, Edward Moringe Sokoine aliweza kuonyesha uzalendo wake na jinsi alivyo na hekima na utayari wa kutetea wasioweza kujitete wenyewe, kwa mfano katika maswali yake ya kwanza kabisa bungeni aliuza: 1.”Kwanini Wamasai wa Ngorongoro wanazuiwa kulima, wakati hawana mifugo ya kuwapatia chakula?” .2 “Kwakuwa tangu kuanza kwa Taifa hili, kuna makabila yamepata maendeleo sana na mengine yapo nyuma sana, je serikali ina mpango gani wa kuwaelimisha walioko nyuma kimaendeleo ili wawe sawa na wenzao?”

Katika hali iliyoonyesha kuaminika mwaka 1967, Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Naibu Waziri, Wizara ya Mawasiliano, Usafirishaji na Kazi n Mwaka 1970, akamteua kuwa Waziri wa Nchi, na Mwaka 1972, Mwalimu Nyerere akamteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Baada ya vyama vya TANU na Afro Shiraz Party (ASP) kuungana na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Februari 5, 1977, Sokoine akawa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Februari 13, 1977 Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Waziri Mkuu, cheo alichodumu nacho hadi anafariki dunia.

Katika vita vya Kagera mwaka 1979, akiwa Waziri Mkuu, Sokoine alikuwa kiungo muhimu, Mwanzoni mwa vita hivyo aliwaagiza Wakuu wa mikoa wote wakusanye nyenzo zote tayari kwa vita ya kupambana na Nduli Idi Amin Dada wa Uganda.

Januari 23, 1979, alitembelea Mtukura jukagua hali ya usalama wakati sa vita hivyo na inaelezwa kwamba wakati wote wa vita Sokoine alikuwa ni nadra kulala usingizi hali inayoekezwa kwamba ilisababisha hadi hali ya afya yake kutetereka.

KUJIUZULU/KUTEULIWA.

Novemba 1980, Sokoine aliomba na kukubaliwa kujiuzulu Uwaziri Mkuu, baada ya kujiuzuku alienda Yugoslavia kwenye matibabu na nafasi yake ikashikwa na Cleopa David Msuya na baada ya kurejea, Mwalimu Nyerere alimteua tena kuwa Waziri Mkuu Februari 24, 1983 na mwaka huo huo wa 1983, Sokoine akaanza kusomea shahada ya “Political Science”.

Aprili 5, 1983, Mwalimu Nyerere alizindua kampeni ya kupambana na wahujumu uchumi baada ya kupitishwa kwa Sheria ya “The Economic Sabotage Act No. 9 of 1983” na kampeni hiyo ambayo ilikuwa ya kufa na kupona akamkabidhi Waziri Mkuu Sokoine kuiendesha na kuisimamia.

Sheria hii ilimtaka mtu aeleze mali aliyokutwa nayo aliipata wapi. Zilianzishwa Mahakama Maalum na Mawakili hawakuruhusiwa kuingia, watu walitakiwa wajitetee wenyewe bila shaka Mwalimu Nyerere aliona kuwa wahalifu wangeweza kutumia ujuzi wa mawakili na kuachiwa.

MCHAPAKAZI.

Katika kutekeleza kampeni hiyo, watu walimuogopa sana Sokoine kiasi kwamba baadhi ya watu katika sehemu nyingi nchini hasa Dar es Salaam, walitupa barabarani na mitaroni vitu vya thamani vilivyokuwa vimeingizwa nchini kinyemela kama Tv na hata Mahindi, maharage na bidhaa nyingine.

Mbali ya bidhaa, wengine walitupa hadi mabunda ya fedha na wapita njia waliogopa kuokota vitu na fedha hizo kwa kumuogopa Sokoine, hivyo Polisi walikuwa wakiziokota fedha hizo na kuzipeleka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na bidhaa kupelekwa kwenye maghala ya Serikali.

Ikumbukwe wakati huo, sheria za nchi zilikuwa haziruhusu mtu binafsi kuwa na duka ka bidhaa yoyote hata vyakula, maduka ya vyakula na bidhaa nyingine yalimilikiwa na Serikali, na yalikuwepo maduka ya Shirika la Biashara la mkoa yaliyoitwa Regional Trading Company (RTC) na hata kwenye usafiri lilikuwepo Kampuni ya Usafiri Tanzania (KAMATA).

Wakati huo ilikuwa ni kosa la kisheria mtu kukutwa na bidhaa kama nguo, sabuni, dawa za kupigia mswaki, mswaki wenyewe na vitu vingine kama hivyo ambapo Sokoine katika mpambano huu dhidi ya wahujumu uchumi ulimjenga sana kisiasa na kumfanya Sokoine kipendwa nchini kote.

Hata hivyo, kulikuwa na malalamiko kutokana na jinsi oparesheni lilivyoendeshwa ambayo yalipelekea Salmin Amour ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani aombe radhi kwa niaba ya Serikali.

Baada ya kifo cha Sokoine, Sheria hii ilifutwa na ikatungwa “The Economic & Organized Crimes Control Act, 1984” ambapo mambo mbalimbali kama uwepo wa mawakili kwenye kesi yalirekebishwa.

BUNGENI.

Aprili 1984 Sokoine alihudhuria Kikao cha Bunge mkoani Dodoma. Jumatatu ya April 9, 1984, Sokoine alikwenda kusali katika Kanisa la Mtakatifu Paul Dofoma. Usiku wa Jumanne, April 10, 1984, aliandaa karamu ya chakula cha jioni kwa Mawaziri na Wakuu wa Mikoa ambapo inaelezwa alionekana kuongea na kila Waziri na kila Mkuu wa Mkoa.

Jumatano, April 11, 1984, aliandaa chakula cha jioni kwa Wabunge wote wa mkoani kwake Arusha ambapo aliwasihi wafanye jitihada kuwaondoa wananchi wao kwenye lindi kubwa la ufukara.

Siku ya Jumatano April 11, 1984, akilivunja Bunge, aliasa kwa uchungu akisema “Ndugu Spika, ningependa kumalizia kwa kukubaliana na Wabunge wote waliosema na ambao hawakusema lakini wana mawazo haya kwamba jambo hili la kutumia fedha bila idhini ya Bunge lazima tutafute kila njia ya kulikomesha”.

Baada ya kulivunja Bunge, katika hali ya kiimani inayoonyesha kuwa Mungu alikuwa ameshapanga jambi lake, Sokoine alipangiwa kusafiri kwa ndege kurudi Dar es Salaam, lakini akakataa, akaamua kusafiri kwa njia ya barabara na sababu ya kufanya hivyo aliiainisha bungeni.

“..Mungu akipenda tutakutana tena kwenye kikao kijacho cha bunge. Mimi nasafiri kwa njia ya barabara ili nijionee hali ya mazao ya wakulima…”, Sokoine akaliambia Bunge.

AJALI/KIFO.

Alhamisi ya April 12, 1984, saa 4:30 asubuhi Sokoine aliondoka na msafara wake kutoka Dodoma, akiongozwa na msafara wa Polisi ambao walikuwa wakihakikisha magari yote yaliyokuwa yakikutana na msafara huo yanaki pembeni kuupisha msafara.

Ni jambo la kawaida kwa misafara ya viongozi kwenda mwendo wa kasi kwa sababu za kiusalama na pia huwa kuna uhakika kwamba hakuna kikwazo njiani kwa kuwa Polisi hutangulia ‘kusafisha’ njia.

Msafara wa Sokoine baada ya kuondoka Dodoma inaekezwa kuwa ulikuwa ukienda kwa spidi ya kilomita 154 kwa saa. Msafara ulipofika eneo la Dakawa mkoani Morogoro, ghafla kilisikika kishindo kikubwa.

Gari la Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine lilikuwa limegongana na gari aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa likiendeshwa na mtu aliyetambuliwa kuwa ni Dumisan Dube, kijana wa umri wa miaka 23, mpigania Uhuru wa Chama cha ANC cha Afrika Kusini, aliyekuwa akiishi Mazimbu, Morogoro.

Ilielezwa kuwa Kijana Dube licha ya kusimamishwa na Polisi, hakusimama kwani nae alikuwa kwenye mwendo wa kasi katika gar lake akuwa na abiria wawili wanaume Boyce Moye na Perce George.

Sokoine, alikuwa amekaa kiti cha nyuma na ilidaiwa hakuwa amefunga mkanda! Masikini, alirushwa toka nyuma hadi akagonga kioo cha mbele na hivyo kusababisha aumie sana na hivyo kufariki dunia kabla ya kufikishwa hospitali ya mkoa wa Morogoro ambako madaktari walithibitisha kifo chake.

Ajali hiyo, ilichukua maisha ya Sokoine tu kwani wengine wote walisalimika na kupata majeraha ya wastani, na ilielezwa kuwa Yusto Chuma, aliyekuwa mlinzi wake ambaye alikaa kiti cha mbele kulia, na Ally Abdalla aliyekuwa dereva wake, walijeruhiwa kiasi.

TANGAZO LA KIFO.

Alasiri ya siku hiyo, Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ghafla ilisitisha matangazo yake na ukapigwa wimbo wa Taifa, Mwalimu Nyerere baada tu ya wimbo huo, kwa uchungu mkubwa, akalitangazia Taifa msiba huo wa kihistoria akasema;

“Ndugu wananchi, leo hii ndugu yetu, kijana wetu, Edward Moringe Sokoine, Waziri Mkuu wa Tanzania, alipokuwa akirejea Dar es Salaam toka Dodoma, gari lake lilipata ajali na amefariki. Ndugu Watanzania naomba muamini Edward amefariki kwa ajali na si kitu kingine”, na baada tu kutoa taarifa hiyo alibubujikwa na machozi kutokana na uchungu.

Baada ya taarifa hiyo jutolewa na Mwalimu Nyerere vilio na simanzi kubwa vilitamalaki nchi nzima. Kwenye maofisi, vyuoni, mashuleni, kwenye mabaa, mabarabarani, kote huko wananchi walionekana dhahiri wameumizwa, hapo Serikali ikatangaza wiki mbili za maombolezo na kuamuru bendera kupepea nusu mlingoti.

Mazishi ya marehemu Sokoine yalipewa heshima zote na yaliyohudhuriwa na umati wa watu wakiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, baadhi ya waliohudhuria ni pamoja na Oliva Tambo aliyekuwa Rais wa ANC na Alfref Nzo aliyekuwa Katibu Mkuu wa ANC ambao inaelezwa kuwa walie lezea kusikitishwa sana na kifo hicho kilichosababishwa na raia mwenzao wa Afrika Kusini. Kufuatia kifo hicho Sokoine aliacha wajane wawili Naponi na Nakiteto na watoto 11.

HUKUMU YA DUBE.

Mei 17, 1984, Dube alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Morogoro ambako kesi yake iliahirishwa. Juni 12, 1984, upande wa mashtaka ukiongozwa na Johnson Mwanyika (SSA) ulifika mahakamani na mashahidi 21. Hata hivyo, Dube aliposomewa mashtaka 7 alikiri yote, Hakimu Simon Kaji (PRM) akampa kifungo cha miaka mitatu.

Kwa jumla ni kwamba kifo cha Sokoine kiliacha kishindo kikubwa sana, sababu yake kubwa ikiwa ni kwamba ni kiongozi ambaye alikuwa amejipambanua katika kujitoa kulitumia taifa la Tanzania kwa uzalendo wa hali ya juu.

Kulingana na wanaomwelezea Sokoine ni kwamba alikuwa mchapakazi, mkweli na muwazi asiyependa uzembe tena mzalendo kwa nchi nchi yake, na uhalisia wake ulijitanabahisha kwa kauli zake mbalimbali anapozungumza na wananchi au viongozi katika matukio mbalimbali kama haya aliyowahi kunukuliwa.

NUKUU.

1. “Ole wake kiongozi asiye na nidhamu na mzembe ntakaemkuta. Viongozi wazembe na wabadhilifu wahesabu siku zao”.

2. “Vijana wengi siku hizi wana mali kuliko wazazi wao waliofanya kazi kwa miaka zaidi ya 40 lakini wazee hao wanataka Serikali ndio iwaulize watoto hao wamepata wapi mali hizo. Mzazi unashindwa nini kumuuliza mwanao?”.

3.”Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi kuwa chombo cha kulinda haki na maslahi ya wengi. Kamwe hayaruhusiwi kuwa chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao”.

4.”Viongozi wanaoteuliwa lazma wawe wazalendo wa hali ya juu. Naskia huko mikoani kuna viongozi wanagombania magari na nyumba. Mambo hayo si muhimu. Viongozi wanatakiwa kugombania juu ya Maendeleo ya wanavijiji. Huu ni ugomvi mtakatifu”.

“Mimi nilikuwa Kamishina wa Planning. Nilikuwa nafanya kazi na makamisha wengine na Sokoine mara nyingine hadi usiku wa manani kisha anatusindikiza ye anarudi kuendelea na kazi. Asubuhi tunakuta ameishatoa mafaili. Marehemu Sokoine alikuwa Mfanyakazi hodari, Mwaminifu na Muungwana sana”. alisema mtu mmoja wa akaribu yake na kunukuliwa katika gazeti moja la Kiingereza la hapa nchini wakati huo.

Hayati Sokoine, japokuwa alipenda maisha bora, lakini hakupenda utajiri, kwani hakuwa na mali yoyote ukiachilia ng’ombe wa urithi. Alikuwa na suti tatu na viatu pea mbili tu”, alinukuliwa Baba wa Taifa akisema kwenye Msiba wa Sokoine ambao aliongoza wakati huo.

Balozi Sokoine amuangukia Rais Samia tatizo la Maji Monduli
AFYA: Vyakula muhimu katika wa msimu wa joto