Lydia Mollel – Morogoro.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damasi Ndumbaro amelitaka Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro pamoja na Uongozi wa Halmashauri hiyo, kuzingatia matumizi sahihi ya maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa shughuli za michezo, ili kufanikisha matengezo na maboresho ya viwanja hivyo.
Dkt. Ndumbaro ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro alipotembelea Kiwanja cha Mchezo wa Gofu cha Gymkana na Dimba la Jamhuri Morogoro, akisisitiza mpango wa serikali wa kufanya ukarabati katika viwanja vitano nchini, ikiwa ni pamoja na Uwanja wa Jamhuri.
Aidha Waziri Ndumbaro ameutaka Uongozi wa Halmashauri Manispaa ya Morogoro kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule za michezo na kuanzisha shule itakayowapokea wanafunzi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya umiseta na umitashumta.
Kwa upande wake Meya Manispaa ya Morogoro, Paschal Kihanga amesema atasimamia kwa weledi maagizo hayo kwa kutenga maeneo ya kujenga shule za michezo na kuanzisha shule itakayotumiwa kwa ajili ya michezo wakati wote.
Naye Mwenyekiti Klabu ya Gymkhana Morogoro, Dkt. Mosi Makao amesema ni mara kadhaa sasa wametoa malalamiko kwa Waziri Ndumbaro kuwa uwanja wao umevamiwa na wanashukuru kwa ujio wake kwani wanamatumani ya kurejeshewa sehemu iliyochukuliwa kwajili ya mazoezi na kujifunzia.