Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini – TAWA, Mabula Nyanda amesema mafanikio yaliyopo katika kudhibiti ujangili kwenye maeneo ya hifadhi, yametokana na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka vipaumbele kwenye eneo hilo na mwitikio wa Wananchi katika kushirikiana na mamlaka.
Akizungumza na Dar24 Media katika mahojiano maalum, Nyanda amesema Rais Samia pia amewezesha taasisi za Hifadhi kutekeleza majukumu yake kiufasaha, ikiwemo kuwapatia rasilimali fedha ambayo imewapa vifaa ikiwemo magari, mahema, silaha na kufanikisha matumizi ya Teknolojia mbalimbali ikiwemo visukuma mawimbi kwa Wanyama, ili kuwafuatilia.
Amesema, “tunapata ushirikiano mkubwa sana Serikalini, na hizo rasilimali fedha zimetuwezesha kwanza kuwa na vifaa (vya kidijitali), sasa hivi sio unaamka tu nyumbani unasema naelekea mahali fulani, mara nyingi tunaamka tukiwa na taarifa za kutosha kwamba mahali fulani kuna dalili ya jambo hili linataka kutokea, kwahiyo mnaenda kulikabili kabla.”
Kuhusu swali lililoulizwa na Mwandishi Stanslaus Lambat juu ya mchango wa Wananchi katika udhibiti wa matukio ya ujangili, Kamishna Nyanda amesema wanashiriki kikamilifu kwani wao ndiyo wana taarifa za uhalifu na wanaojihusisha na ujangili baadhi wanatoka katika maeneo wanayoishi, hivyo inakuwa rahisi kumaliza tatizo.
“Kwahiyo wananchi wanahusika sana kutoa taarifa pale (ujangili) unapotaka kutokea, lakini kwasasa kutokana na Wananchi walivyohamasika wanazoziona faida za rasilimali za Wanyamapori na elimu inayotolewa wameshajua umuhimu wa uhifadhi, na wakati mwingine wamekuwa mstari wa mbele kuisaidia Serikali kupambana na vitendo vya ujangili,” amesema Kamishna Nyanda.
Wanyamapori ni maliasili iliyo na umuhimu mkubwa kibiolojia, kiuchumi katika kusafisha mazingira, kuboresha hali ya hewa, kuhifadhi maji, ardhi na virutubisho ambavyo havina budi kuhifadhiwa ambapo Mamlaka zake zina jukumu la kupambana na matumizi haramu yanayofanywa na watu wenye nia ovu.