Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi ameagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi – OSHA, kuongeza jitihada katika kuwaelimisha na kuwahamasisha wadau wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi, ili waweze kutekeleza sheria na miongozo mbalimbali ya usalama na afya kwa hiari.

Ndejembi ametoa agizo hilo bada ya kufanya ziara katika Ofisi za OSHA, Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza jinsi Taasisi hiyo iliyopo chini ya Wizara yake inavyotekeleza majukumu yake, ambapo baada ya kusikiliza wasilisho la Mtendaji Mkuu, Khadija Mwenda kuhusu OSHA na majukumu yake, akaitaka menejimenti kuwekeza katika mifumo kidijitali, ili kurahisisha utendaji na kuongeza ufanisi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi.

Amesema, “nimejifunza mengi kutokana na wasilisho la Mtendaji Mkuu hivyo ninawashauri kuwekeza zaidi katika mifumo ya TEHAMA pamoja na kubuni mikakati ya kuongeza uelewa miongoni mwa wadau wenu na wananchi kwa ujumla ambao uelewa wao kuhusu masuala haya bado ni mdogo.”

Aidha, Ndejembi pia alishuhudia utiaji saini wa Hati ya Mashirikiano baina ya OSHA na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania – TUGHE, yatakayoziwezesha Taasisi hizo mbili kushirikiana katika mambo mbali mbali hususan suala la utoaji elimu ya usalama na afya kwa Wanachama.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, pamoja na kuwasilisha mada kuhusu utendaji wa OSHA katika kikao hicho, amempongeza Waziri Ndejembi kwa kuteuliwa kuiongoza Wizara ya Kazi na Ajira na amemuahidi kuhakikisha Taasisi hiyo inatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Casimiro kukimbilia Saudi Arabia
Simba SC kufunga hesabu kwa Ayoub Lakred