Rais wa Iran Ebrahim Raisi (63), Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo, Amir Abdollahian na Maafisa wengine saba waliokuwamo kwenye msafara wamepatikana wakiwa wamefariki katika eneo la ajali ya Helikopta iliyoanguka katika eneo la Jolfa, lililopo zaidi ya kilomita 600 kutoka Tehran karibu na mpaka wa jimbo la kaskazini-magharibi mwa Azerbaijan wakati wakitokea katika mkutano na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la Iran la Mehr la Nchini Iran, limeripoti kuwa, Helikopta hiyo ilitoweka kwenye rada Jumapili mchana na katika ajali hiyo hakuna mtu aliyenusurika na Serikali ya Iran bado haijatia neno kuhusiana na tukio hilo.
Mkuu wa shirika la Hilali Nyekundu la Irani, Pirhossein Koolivand amesema timu za waokoaji ziliyafikia mabaki ya helikopta hiyo na kudai kuwa kutokana na hali mbaya ya hewa iliwachukua masaa mengi kwani ulikuwepo ukungu na ugumu wa kupita kwenye eneo la misitu na milima iliyochangia kutatiza shughuli za uokozi
Nchi kadhaa zikiwemo Urusi na Uturuki zimetoa msaada katika operesheni ya uokoaji, huku ndege isiyo na rubani ya Uturuki pia ikiruka katika anga ya Iran kusaidia shughuli ya utafutaji, huku Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei akitoa wito kwa Wairan kumwombea Raisi.
Raisi ambaye alizaliwa mwaka wa 1960 huko Mashhad, kaskazini-mashariki mwa Iran, aliapishwa kuwa rais mpya wa Iran Agosti 2021 na alishinda uchaguzi wa urais chini ya asilimia 62 ya kura kama mgombea mkuu wa vyama vya siasa kali na anayependwa zaidi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa katiba ya Iran, Raisi alikuwa ni Kiongozi wa pili kinyadhifa, chini ya Khamenei ambaye ni Mkuu wa nchi na pia ndiye mwenye uamuzi wa mwisho katika masuala yote ya kimkakati.