Scolastica Msewa, Kibaha – Pwani.
Wakala wa Vipimo Tanzania – WMA, umesema upo tayari kutoa ushirikiano kwa Wananchi wenye mashaka au changamoto yoyote ya Vipimo kwa lengo la kujiletea maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Wakala huo Mkoa wa kihuduma Misugusugu, Charles Mavunde wakati wa maadhimisho ya siku ya Vipimo duniani iliyofanyika katika viwanja vya Misugusugu Kibaha Mkoani Pwani.
Amesema, “Wakala wa Vipimo Tanzania wapo tayari kutoa ushirikiano kwa wananchi wenye mashaka au changamoto ya dira za maji, mizani ya maduka, mita za umeme, matanki ya magari yabebayo vimiminika ili kutoa huduma na kuuza bidhaa zenye ujazo, uzito na urefu unaoenda na thamani ya fedha ya mteja.”
Aidha, Mavunde aliwataka Waandishi wa Habari kuendelea kutoa ushirikiano wa kuelimisha jamii kuhusu jamii kuhusu Wakala wa Vipimo ili kumletea Mwananchi maendeleo kama kauli mbiu ya mwaka huu ya Maadhimisho ya siku ya Vipimo duniani inayosema “Tunapima leo kwa kesho endelevu”
“Hii ni hatua ya kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020 ambayo inataka katika sekta ya maji inataka kufikisha huduma kwa jamii kwa mijini asilimia 95 na asilimia 85 vijijini ifikapo mwaka 2025 pia kuboresha huduma za umeme mijini na vijijini kupitia REA na kuboresha Nishati ya mafuta na gasi” alisema Mavunde.
Awali, Diwani wa Kata ya Misugusugu, Upendo Ngonyani ambaye alikuwa Mgeni rasmi aliwataka Wadau wa vyombo vya usafirishaji wa vimiminika, kuisaidia Serikali kupima matanki ya magari yabebayo vimiminika, ili kutoa Vipimo sahihi kwa Wananchi.