Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) kununua mpunga kwa bei ya Shilingi 900 kutoka 570, ambayo itakuwa na tija kwa Mkulima.
Rais Samia amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Ifakara katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa CCM Ifakara Mji, Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro.
Amesema, pia Serikali itaendelea kuwapelekea wakulima wa Kilombero pembejeo za kilimo na kukamilisha miradi ya umwagiliaji inayotekelezwa, ili kuwaongezea tija katika kilimo.
Aidha, Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa Serikali inafanyia kazi miradi mbalimbali Wilayani hapo ikiwemo kukarabati skimu ya Idete pamoja na kuchimba na kujenga miundombinu ya maji ya Kilombero Block Farm.
Amewahimiza pia wananchi hao kuzalisha kwa wingi kwa kuwa soko lipo na Serikali inatoa ruzuku huku akiwataka kujiwekea akiba wanapopata fedha za mavuno na pia kujikatia bima ya afya, ili wao na familia zao wanufaike na huduma za afya zilizoboreshwa mwaka mzima.
#RaisSamiaZiaraMoro