Timu maalum ya kupambana na makosa ya mtandao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano TCRA, wamewakamata watuhumiwa 20 wakiwemo raia wanne wa Nchi jirani kwa makosa ya kuingilia mifumo ya mawasiliano.
Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti Mkoani Arusha Oktoba 2024.
Amebainisha kuwa, watuhumiwa 16 kati ya waliokamatwa ni mawakala wa kusajili laini za mitandao ya simu kwa kutumia vitambulisho vya Taifa NIDA vya watu wengine bila ridhaa zao, na kisha kuuza kwa wahalifu hao ambao huzitumia kuingilia mifumo ya mawasiliano na kufanya uhalifu.
Aidha katika ufuatiliaji walibaini kuwa laini nyingi wameziuza kwa raia hao wanne wa Nchi Jirani ambao walikutwa na mitambo ya mawasiliano aina ya Simbox, Laini mbalimbali za mitandao ya simu, kompyuta mpakato, komptyuta, simu za mikononi, invetor solar na betri za solar.
Kamanda Masejo amesema upelelezi wa shauri hilo umekamilika, na taratibu nyingine za kisheria zinafuata huku akitoa wito kwa watu wanaosajili laini za simu ambao sio waaminifu wanaotumia vitambulisho vya Taifa vya watu wengine kusajili laini na kuuza kwa watu wengine kuacha mara moja kwani wataendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi yayao.
Amewataka pia wamiliki wa nyumba kuwa makini na wapangaji wanaowapangisha katika nyumba zao, kwani baadhi ya wahalifu hutumia nyumba hizo kufanya vitendo vya kihalifu.