Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeagizwa kuongeza kasi ya kupunguza tatizo la uhalifu mtandaoni.
Agizo hilo limetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Januari 20, 2025 Bungeni jijini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati hiyo cha kupokea na kujadili taarifa ya utelekezaji wa Bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso ameipongeza wizara hiyo pamoja na taasisi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kazi nzuri ya kuboresha Uchumi wa kidijitali na kudhibiti uhalifu wa mtandaoni.
Aidha, Kamati ilishauri wizara kuzisimamia kampuni za simu kuhakikisha kuwa anayesajili laini ni mhusika halali, na kuzuia tabia ya watu kusajili laini kwa niaba ya watu wengine ili kudhibiti laini hizo kutumika kufanya uhalifu wa mtandaoni.
Kwa kuzingatia kukua kwa teknolojia zinazoibukia na matumizi ya Akili mnemba, Kamati hiyo imeiagiza Wizara kusimamia matumizi ya teknolojia zinazoibukia ili zisitumike vibaya ila zisaidie kupunguza uhalifu mtandaoni.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry William Silaa alisema kuwa anga la mtandao la Tanzania ni salama na kwamba nchi imeendelea kufanya vizuri katika kanda ya Afrika.
Waziri Silaa alieleza kuwa hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa, na kwamba Wizara anayoisimamia pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi zilikutana mwishoni mwa mwaka 2024 na kuahidi kuongeza kasi zaidi katika kudhibiti uhalifu mtandaoni.
Waziri Silaa alibainisha kuwa Wizara imefanikiwa kutoa elimu kwa umma kwa wananchi kupitia mitandao ya kijamii na vituo vya redio na televisheni ambapo takribani wananchi millioni tatu (3,000,000) wamepata elimu kuhusu ulinzi na usalama wa mtandao katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, na Zanzibar walifikiwa.