Watanzania wanaoishi Jamhuri ya Czech wameahidi kushirikiana na Serikali kuchangamkia fursa zinazopatikana katika nchi hiyo kwa manufaa ya nchi na wananchi.

Ahadi hiyo wameitoa hivi karibuni, walipofanya kikao na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo katika mji wa Brno, Czech.

Wamesema Czech ni nchi iliyopiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo za elimu na ufundi, hivyo, wameishauri Serikali kuchangamkia nafasi za ufadhili wa masomo zinazotolewa na Serikali hiyo ili Watanzania wengi waweze kufaidika.

Wamesema Fursa za ajira Czech bado zipo, hivyo kwa wale watakaobahatika kupata ufadhili wa masomo na wakipenda kuendelea kuishi Czech uwezekano wa kupata ajira ni mkubwa.

Kwenye upande wa kutangaza utamaduni na lugha ya Kiswahili, waliishauri Serikali njia nyepesi ya kutangaza utamaduni wa Kiswahili ni kuingiza vitabu vingi kwenye nchi hiyo na kuvitafsiri kwa kuwa wananchi wa Czech wanapenda sana kusoma vitabu.

Waliiomba Serikali iangalie uwezekano wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kushiriki katika zoezi la kupiga kura kwani wengi wao bado ni raia wa Tanzania. Aidha, waliiomba Serikali iwasadie kurejesha miili nchini Tanzania kwa watakaofariki dunia nje ya nchi na kupenda kuzikwa nyumbani.

Kwa upande wake, Waziri Kombo alifurahishwa na ushauri uliotolewa na diaspora hao ambao umejikita katika kujenga nchi. Alisema wao ndiyo daraja na mabalozi wazuri kwa sababu wanaishi katika jamii, hivyo ni jukumu lao kuitangaza nchi kwa matendo na tabia nzuri na wanaponusa fursa ni vizuri wakaijulisha Serikali kupita ofisi za Balozi.

“Tunao ubalozi wetu hapa Czech unaowakilisha kutokea Berlin, Ujerumani chini ya Mhe. Balozi Hassani Mwamweta na Mwakilishi wetu wa Heshima hapa Brno, Roman Grolig wanafanya kazi nzuri nawasihi muwatumie wakati wote”, Waziri Kombo alisema.

Alisifu pia jitihada za diaspora waliopo mji huo kwa kuweza kufika nchini humo wengi wakifuata fursa za masomo kwenye fani tofautitofauti zenye manufaa kwa nchi. Fani hizo ni biolojia ‘Molecular Cell Biology’ uhandisi wa mitambo ‘Electro Mechanic’ pamoja na sayansi ya michezo ‘ Physical Education on Coaching SoftBall’.

Kuhusu kurejesha miili ya Marehemu nyumbani, Waziri Kombo alishauri zitumike njia zilizopo zikiwemo kukata bima na kwamba Serikali kupitia ofisi za Balozi itahakikisha vibali vyote muhimu vya kusafirisha miili vinapatikana.

Alimalizia kwa kufafanua kuwa suala la kupiga kura kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni bado halijatungiwa Sheria isipokuwa kwa sasa, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha hadhi maalum kwa diaspora.

Kyler walker akubali kuishi nje ya Manchester City kwa miezi 12
Lewis Hamilton ameanza kwa kishindo Ferrari baada ya kuitosa Mercedes Benz