Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuweka miundombinu ya kutumia gesi asilia (CNG) katika magari ya serikali ili yaweze kuanza kutumia nishati ya gesi.
Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan kwa niaba ya Waziri wa Nishati, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega aliyeuliza mkakati wa wa Serikali kuhakikisha Magari ya Serikali yanakuwa na mfumo wa nishati ya gesi.
“Mhe. Spika Ili kuwezesha Serikali kuanza kutumia magari yanayotumia gesi, Serikali imejikita kuweka miundombinu ya kuwezesha matumizi ya CNG kwenye magari ya serikali kwa urahisi,”  amesema Kitandula.
Kitandula ameongeza kuwa Serikali kupitia GPSA (The Government Procurement Services Agency) imeshaanza taratibu za kuweka miundombinu kwa ajili ya magari ya serikali yatakayo tumia gesi ikiwemo kufanya tathimini za athari za Kijamii na mazingira pamoja na uandaji wa michoro ya kina ya kihandisi na usimamizi wa ujenzi.
Amezielezea taratibu hizo kuwa ni kuweka miundombinu rafiki kwa magari ya serikali kuanza kutumia gesi kwenye magari (CNG).
Aidha, ili kuboresha upatikanaji wa CNG kwa mikoa iliyo katika barabara kuu kuelekea Dodoma, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ipo kwenye hatua za manunuzi za mradi wa kuagiza na kusimika vituo vya CNG vinavyohamishika ambapo kwa kuanzia vitatu vitasimikwa Dar es Salaam, kimoja kitasimikwa Morogoro na viwili vitasimikwa Dodoma.
Hatua hizi ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuboresha nishati rafiki kwa mazingira na kuongeza ufanisi katika matumizi ya gesi, Vituo vya CNG vitasaidia serikali na wananchi katika kufikia malengo ya matumizi ya nishati bora ikiwa Serikali inaamini kuwa matumizi ya gesi asilia katika magari ya serikali yatasaidia kupunguza matumizi ya mafuta ya petroli na hivyo kupunguza gharama za nishati.

Kuna fursa nyingi za uwekezaji Zanzibar - Rais Dkt. Mwinyi
Dunia yakaribishwa kuwekeza kwenye sekta ya Nishati Nchini