Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imeeleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), katika kusimiamia utekelezaji wa ujenzi wa minara 758 inayojengwa katika kata 713 nchini licha ya changamoto za ubovu wa barabara zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 52.4.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Holle baada ya kamati kutembelea na kukagua ujenzi wa minara katika kata ya Esilalei na Sepeko, wilayani Monduli, mkoani Arusha, ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa uwekezaji huo unakuwa wenye tija.
Holle ameongeza kuwa, licha ya mafanikio hayo UCSAF ina wajibu wa kuendelea kusimamia na kufanya ufuatiliaji kwani maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa watoa huduma wanakamilisha ujenzi wa minara yote ifikapo Mei 13, 2025 kama ilivyo ilivyoainishwa katika mikataba, na kuwa Serikali haitaongeza muda wa utekelezaji wa mradi huo.
“Tunajua maelekezo ya Rais ni kuwa mradi huu hautaongezewa muda, na sisi kama Kamati tunapenda kusisitiza hapo, wasimamieni watoa huduma wakamilishe kwa wakati ili tija ya uwekezaji huu uonekane kwa wananchi kwa kuanza kupata mawasiliano,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utafiti Mhandisi Albert Richard amesema, kupitia mradi huo jumla ya minara 141 inajengwa katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Manyara.
Naye mkazi wa kijiji cha Sepeko, Letema Saning’o amesema kabla ya kuanza kupata mawasiliano walikuwa wakiteseka kwa kutembea umbali mrefu kufuata mtandao, lakini sasa anaishukuru Serikali kwani tangu mnara huu uanze kutoa huduma hawana tena uchangamoto ya mawasiliano. Kwa upande wake Kadogo Maenga, mkazi wa Esilalei, amesema kwa sasa hawatafuti tena mbinu mbadala za kupata mawasiliano tangu mnara huo ulipoanza kutoa huduma.
Serikali kupitia UCSAF imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 126 kwa makampuni ya simu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu ili kufikisha mawasiliano kwa wananchi wapatao milioni 8.5. Hadi sasa Serikali imeshalipa kiasi cha shilingi bilioni 70 ili kuwezesha watoa huduma kuagiza vifaa vya ujenzi wa minara kwa kuwa asilimia kubwa ya vifaa huagizwa nje ya nchi.