Tanzania imependekeza kusaini Hati ya Makubaliano na Comoro kuhusu ushirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji hususan katika eneo la kulinda uwekezaji na biashara, inayolenga kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji na wafanyabiashara hususan za ukiukwaji wa makubaliano wanayoingia.

Hayo yamejiri wakati wa kikao kati ya Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Saidi Yakubu na Waziri wa Uchumi, Viwanda na Uwekezaji wa Comoro, Moustoifa Hassani Mohamed kilichofanyika katika ofisi za Wizara hiyo Februari 20, 2025

Balozi alishauri serikali ya Comoro kuanzisha eneo maalum la kiuchumi kama ilivyo EPZ kwa Tanzania litakalosaidia upatikanaji wa bidhaa kirahisi. Alisema hatua hiyo itakuwa ni moja ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Marais walipokutana pembezeni mwa Mkutano wa Nishati ambapo walisisitiza umuhimu wa kuweka mazingira wezeshi ili kurahisisha biashara baina ya mataifa haya mawili.

Aidha, alitumia fursa hiyo, kumkaribisha Waziri na wataalam wake kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania ili kukutana na wenzao na kuona namna bora ya kuandaa makubaliano pendekezwa.

Alisema kuwa ziara hiyo itatoa fursa pia ya Serikali yake kujionea namna Wacomoro wanavyofanya biashara nchini Tanzania na kusikiliza kero na changamoto zao pamoja na kutembelea eneo la EPZ, Ubungo.

Moustoifa aliunga mkono mapendekezo hayo na kueleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kindugu na wa muda mrefu kati ya Tanzania na Comoro hususan eneo la biashara.

Waziri alijulisha kuwa, tayari kikao cha Mawaziri wa sekta husika kimefanyika cha kuweka mikakati ya utekelezaji wa maelekeo ya Waheshimiwa Marais ambayo ni pamoja na kukamilisha taratibu za kuwa na Mwambata Uchumi katika Ubalozi wa Comoro nchini Tanzania.

Wafula Chebukati wa IEBC Kenya aaga dunia
Maisha: Mbinu ya kumpata mpenzi wa ndoto zako