Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ustawi wa Jamii katika Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais ā€“ TAMISEMI, Subisya Kabuje ametoa wito kwa wadau wanaotoa misaada kwa wanawake na vijana wa kike kuhakikisha wanawahusisha pia vijana wa kiume na wanaume katika vikundi vya maendeleo, ili kuimarisha ustawi wa familia na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Kabuje ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kukagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika la Brac Maendeleo katika Wilaya ya Singida Vijijini, mkoani humo.
Ameeleza kuwa vikundi hivyo vimekuwa vikipatiwa elimu na misaada mbalimbali, ikiwemo mafunzo ya ujasiriamali, ufugaji na usimamizi wa fedha, ili kusaidia familia zenye kipato cha chini kujikwamua kiuchumi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wataalamu wa maendeleo ngazi ya mkoa, halmashauri na vijiji kushiriki kikamilifu katika kusimamia uwekezaji wa miradi hiyo, kwani inasaidia jamii kupambana na umaskini.
Vilevile, Kabuje amewahimiza wazazi kuanzisha vituo vya kijamii vya kulelea watoto wadogo walio chini ya miaka mitano ili kuwasaidia wakati wanapokuwa kwenye shughuli za biashara au kilimo. Vituo hivyo vitatoa huduma muhimu za lishe, afya, ulinzi na ujifunzaji wa awali kwa watoto.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo, Rachel Mbwiliza, amesema mradi huo unalenga kusaidia watu wa rika mbalimbali, huku hatua ya awali ikitekelezwa katika Halmashauri za Wilaya ya Manyoni, Chamwino, na Singida Vijijini.

Lamine Yamal afichua siri kuelekea droo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
Mabosi wa Tottenham wakoshwa na Andoni Iraola