Johansen Buberwa – Kagera
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa zoezi la upandaji vifaranga vya samaki Mil.1.5 kwenye Ziwa Ikimba lililopo mkoani Kagera litaongeza mavuno ya Samaki kwa mwaka kwenye ziwa hilo kutoka Tani 1 inayovunwa hivi sasa hadi tani 13 baada ya miezi 6.
Dkt. Kijaji amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa upandaji wa vifaranga hivyo na kukabidhi boti moja ya doria kwenye mwalo wa Buterankuzi ambapo amewataka wananchi wa kata zote zinazonufaika na ziwa hilo kulinda vifaranga hivyo ili waweze kunufaika na mavuno kwenye ziwa hilo.
“Lakini pia naelekeza wataalam wangu kabla hamjaondoa, mfanye tathmini kama ndani ya Ziwa Ikimba kunaweza kufanyika ufugaji wa vizimba ili wananchi hawa wanufaike zaidi na uwepo wa ziwa hili” amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji ametumia fursa hiyo kutangaza upumzishwaji wa ziwa hilo kwa miezi 6 ili kuvipa nafasi vifaranga hivyo kukua hadi kufikia hatua ya matumizi kibiashara huku pia akitangaza kufanyika kwa doria ya wakati wote kwa ajili ya ulinzi wa rasilimali zilizopo kwenye ziwa hilo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kaibanja Jasson Rwankomezi amesema kuwa hali ya upatikanaji wa samaki katika ziwa hilo kwa sasa haikidhi hata mahitaji ya chakula hivyo wananchi wameamua kwa hiyari zoezi hilo ili waweze kunufaika kijamii na kukuza uchumi wao.
Nao baadhi ya wavuvi waliozungumza na Dar 24 media akiwemo Anton mussa na Donatus Ishemo wameishukuru serikali kwa hatua hiyo wakiwa wanatarajia ziwa likifunguliwa watapata furusa za kupata samaki wengi wa kutosha hali itakayowainua kiuchumi.