Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) na Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) itaanzisha teknolojia ya kuchakata migomba kwa ajili ya chakula cha mifugo na viwanda vya kutengeneza mvinyo, unga wa lishe, keki na vipande vinavyotokana na ndizi.

Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma hii leo Aprili 10, 2025 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Buhigwe Kavejuru Eliadory aliyeuliza Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Viwanda vya kuchakata zao la Migomba.

“Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua umuhimu wa uongezaji thamani zao la migomba pamoja na ndizi, Serikali kupitia SIDO imepanga kuanzisha Kongani ya zao la migomba/ndizi katika Halmashauri ya Buhigwe,” alijibu Kigahe.

Amesema, “mpango huo unatarajiwa kuanza ifikapo Julai, 2025 kwa majadiliano kati ya SIDO na Halmashauri ya Buhigwe ili kukubaliana eneo ambalo Kongano hiyo itawekwa pamoja na gharama za programu hiyo.”

Naibu Waziri huyo amesema Kutokana na tafiti zilizofanywa duniani, zao la migomba lina faida nyingi ikiwa ni pamoja na kutumika kutengeneza bidhaa za asili kama vile vikapu, mikeka na kofia.

“Zao hilo hutumika kutengeneza chakula cha mifugo, mbolea, nguo, karatasi, nishati ya kupikia, dawa za asili na malighafi za kujengea,” amesema.

“Hivyo, zao hili ni miongozi mwa rasilimali zinazopatikana nchini zitakazoongezewa thamani kupitia Mpango Maalum wa Kuendeleza Viwanda wa Miaka Mitano (5) unaotarajiwa kutekelezwa kuanzia Mwaka wa Fedha 2025/26 hadi 2029/30,” amesema Kigahe.

Polisi: Lissu amekamatwa kwa tuhuma za uchochezi
DC Kubecha azigusa Taasisi za Kijamii, Vyombo vya dola