Serikali kupitia Mradi wa Grid Imara inaendelea na Ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mkata-Handeni ambapo kwa sasa mkandarasi yupo kwenye hatua za awali za ujenzi (site clearance).

Ameyazungumza hayo hii leo Bungeni Jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga wakati akijibu swali la Mbunge wa Handeni Mjini Reuben Kwagilwa aliyeuliza Je, Serikali ina maelezo gani juu ya kero sugu ya kukatika umeme mara kwa mara Handeni Mjini na ni lini kero hiyo itatatuliwa.

“Changamoto ya kukatika umeme Wilayani Handeni inatokana na uchakavu wa miundombinu ya kusambaza umeme pamoja na urefu wa njia za kusambaza umeme,” amesema.

“Katika kukabiliana na changamoto hii, Serikali kupitia TANESCO inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya umeme ikiwa ni pamoja na kubadilisha nguzo za miti na kuweka za zege,” qmesema Kapinga

Aidha amesema, ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kilindi umefikia asilimia 35 na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovolt 132 kutoka Mkata, Handeni hadi Kilindi umefikia asilimia 30.

“Kukamilika kwa kazi hizi kutawezesha kuondoa kero sugu ya kukatika umeme Handeni Mjini,” amesema Kapinga.

Wakurugenzi zingatieni taratibu za kiutumishi - Mchengerwa
M23, DRC waahirisha mazungumzo ya kusaka suluhu