Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kibaha na Chuo Cha Uongozi wa Elimu ADEM wanatarajia kuja na mpango wa pamoja wa kutoa mafunzo kwa walimu nchi nzima, ili kuboresha sekta ya elimu na kujenga uzalendo kwa walimu na wanafunzi nchini.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Chuo Cha Uongozi wa Elimu ADEM Dkt. Maulid Maulid aliyekuwa mgeni rasmi wa kufunga Mafunzo ya siku tatu kuwajengea uwezo Walimu wakuu wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam yaliyofanyika katika Shule ya uongozi ya Mwalimu Nyerere Kibaha ambapo Walimu wakuu 76 kutoka katika chama Cha Walimu wakuu TAHOSSA wameshiriki.
Dkt. Maulid amesema wanekubaliana na Shule ya Mwalimu Julius Nyerere waanzishe utaratuibu wa kutoa mafunzo kwa Walimu ya muda wa wiki moja ili waweze kuiva zaidi ambayo watahakikisha Walimu wote nchi nzima wanahudhuria.

Alisema, Chuo cha ADEM wanatoa elimu ya Uongozi kwa Walimu lakini Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kibaha wao wanatoa elimu ya Uongozi kwa ujumla na Wana miundo mbinu bora kwa malazi ya Walimu.
Akizungumzia suala la kuthibiti vitendo vya ukatili kwa watoto Dkt. Maulid amesema kuthibiti wa vitendo vya ukatili kila mtu ananafasi yake kuanzia ngazi ya familia, majirani serikali ya mtaa na mamlaka nyingine zote mimi naisihi jamii na mamlaka wasimamizi wa elimu kuhakikisha usalama wa Wanafunzi na watoto kwa ujumla.
“Ukatili kwa watoto wanafunzi
Changamoto za afya ya akili zinachangia waalimu kutoa adhabu kali kwa wanafunzi hivyo tumeamua tuanzishe mpango wa kuwapa mafunzo ya mara kwa mara na kuwasisitiza miiko ya uongozi hasa kwa waalimu wakuu,” alisema Dkt. Maulid.

“Taasisi zote zinazosimamia watoto wote tuwajibike kwa pamoja kuanzia wakuu wa shule na waalimu wa madarasa ambao wamekuwa wakiwafuatilia watoto ambao wamekua wakifanyiwa ukatili kutoka majumbani tuwapongeze waalimu hao kwani nao wamekua wakifanya kazi kubwa” amesema Dkt. Maulid.
Kaimu Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere ya Kibaha mkoani Pwani John Baitan amesema Mafunzo hayo kwa Viongozi wa shule pia watajifunza kuhusu Usalama wa nchi, Itifaki, uzalendo, Umajumui, usimamizi wa fedha za serikali na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato kwa Viongozi wa shule za sekondari ikiwa ni katika kuwajengea uwezo wa kiutendaji wa kazi zao za kila siku mashuleni.